Skip to main content

ALIYESHINDA RUFAA NA KUTOKA JELA AKAMATWA KWA UJAMBAZI SUGU DAR

ALIYESHINDA RUFAA NA KUTOKA JELA AKAMATWA KWA UJAMBAZI SUGU DAR.




Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mtuhumiwa anayedaiwa kuwa ni jambazi sugu anaejukina kwa jina la Jonson Omary Mchome (39) dereva wa bodaboda.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 25, 2022 jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari.

ACP Muliro amesema kwamba mtuhumiwa huyo amekuwa akituhumiwa kujihusisha na vitendo vya kiharifu katika maeneo mbalimbali pamoja na wenzake.

"Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyu maeneo ya Kwembe katikati ya Kwembe na Kisarawe katika Wilaya ya Ubungo na kukamatwa kwake kulitokana na Wananchi wema kutoa taarifa ambazo zilifatiliwa kwa haraka na Makachero wa Jeshi la Polisi na mtuhumiwa huyu ambae wakati mwengine mitaani anatumia jina tofauti na lililopo katika kitambulisho cha mpiga kura pamoja na hati ya kusafiria ambapo mtaani anajulikana kwa jina la Athumani Rashidi Amir"amesema ACP Murilo.

Kadhalika ACP Muliro amesema baada ya mtuhumiwa kubaini kuwa anafatiliwa na Jeshi la Polisi na amezingirwa alitoa Bastola kwenye begi na kuanza kuwashambulia Askari ambao nao walijihami kwa kumshambulia na kumpiga risasi moja katika mguu.

"Katika hali hiyo Askari walifanikiwa kuipata Bastola moja aina ya feth 13 ambayo ilikuwa na namba T 062010J004070 ambayo ilitengenezwa Uturuki ilikuwa na namba za usajiri za Tanzania TZ 95973 ambayo ilikuwa na risasi moja,” amesema ACP Morilo.

Aidha ACP Murilo amesema ufatiliaji wa haraka wa Jeshi la Polisi ulibaini kuwa Bastola hiyo iliporwa eneo la Chanika ambapo waliwahi kufanya tukio  wakiwa na mapanga wakafanikiwa kupora pesa katika moja ya nyumba pamoja na  Bastola hiyo baada ya kumjeruhi kwa panga mmiliki.

"Mtuhumiwa huyu alihojiwa kwa kina zaidi na alieleza yeye pamoja na wenzake wamekuwa wakifanya matukio hayo mwaka huu kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam,kutokana na jeraha alilolupata mtuhumiwa amekimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili keaajili ya matibabu na aweze kufanyiwa mahojiano baada ya kupona,” ameongeza ACP Muliro.

Comments