KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA WATOTO DUNIANI,BARAZA LA WATOTO LATAKA USIMAMIZI THABITI WA HAKI ZA WATOTO NCHINI.
KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA WATOTO DUNIANI,BARAZA LA WATOTO KINONDONI LATAKA USIMAMIZI THABITI WA HAKI ZA WATOTO NCHINI.
Kuelekea maadhimisho ya kimataifa ya siku ya watoto duniani ambayo huadhimishwa Novemba 20 kila mwaka,baraza la watoto manispaa ya Kinondoni limeipongeza serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa inayofanyika katika kuhakikisha watoto wanapata elimu,huduma za afya,pamoja na kuweka mifumo mbalimbali ya ushirikishwaji wa watoto kama vile mabaraza ya watoto.
Wakizungumza
na waandishi wa habari leo Novemba 19,2022 katika ofisi za shirika la
Save the Childrens Tanzania, jijini Dar es salaam viongozi mbalimbali wa
baraza hilo wamesema kuwa hatua ya serikali kutunga sera na miongozo
mbalimbali ya kulinda na kusimamia haki za watoto kama vile sheria na
sera ya mtoto na hivi karibuni muongozo wa uanzishwaji wa madawati ya
ulinzi wa watoto ndani na nje ya shule ni hatua ya kupongezwa
itakayochochea kuwepo kwa haki za watoto.
Mwenyekiti
wa baraza hilo la watoto wa manispaa ya Kinondoni,Rahabu Fransis
amesema kuwa pomoja na kwamba Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa
inayoitaka kulinda haki ya watoto,bado sheria ya ndoa ya mwaka 1971
inayoruhusu watoto kuolewa chini ya miaka 18 huku michakato ya
urekebishaji wa sheria hiyo ikiwa mingi na mirefu na kuwaacha watoto wa
kike wakiendelea kuumia,hivyo baraza hilo linaihimiza serikali
kuharakisha mabadiliko ya sheria hiyo ya ndoa ili kulinda watoto,hasa wa
kike hapa nchini.
"vile
vile tunaiomba serikali iweke miundombinu rafiki itakayowawezesha watoto
hasa wenye ulemavu kupata elimu,Hii ni pamoja na kujenga madarasa ya
kutosha,madawati,kufunza walimu wa elimu maalum na kuweka mifumo ya
usaidizi itakayowezesha elimu sawa kwa wote." amesema Rahabu
Kwa
upande wake Sabrina Juma Salum ambaye ni kiongozi wa nidhamu kwa watoto
wa kike wa baraza hilo la watoto manispaa ya Kinondoni amesema kuwa
licha ya serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Rais Samia
Suluhu Hassan kutoa muongozo wa kurudi shule hasa kwa wanafunzi
walioacha masomo kutokana na kupata ujauzito bado inahitajika serikali
na wadau mbalimbali kutoa elimu juu ya muongozo huo ili watoto hao
waweze kusaidiwa kurudi mashuleni.
Amesema
kuwa serikali iweke mazingira mazuri ya watoto wanaopata ujauzito
kurudi katika mfumo rasmi wa masomo ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo
mashuleni ya utoaji ushauri nasaha,na kutoa kwa jamii ili iweze kutambua
kuwa mtoto anayepata ujauzito bado ni mtoto na ana haki ya kuendelea na
masomo.
Kuhusu masuala
ya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto,katibu wa baraza hilo la
watoto Miraji Idrisa amesema kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa dhidi ya
watoto,majumbani,kwenye jamii na mashuleni ikiwemo
kupigwa,ubakaji,matusi, kutelekezwa na kutengwa vimewaathiri watoto
kimwili na kisaikolojia pamoja na kuathiri ustawi wa watoto ,hivyo
ameiomba serikali kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kufanya vitendo
hivyo na kama watoto watakuwa tayari kutoa taarifa pale watakapoona
vitendo hivyo vikifanyika.
Kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi
,Sadiki
H Sadiki ambaye ni afisa habari wa baraza hilo la watoto amesema kuwa
majanga yatokanayo na mabadiliko hayo yamekuwa yakiwaathiri watoto.
"Sisi
kama watoto tayari tumeona mabadiliko ya tabia ya nchi yakituathiri,kwa
mfano sasa jukumu la kutafuta maji ambalo linatokana na ukame wa muda
mrefu kwa kiasi kikubwa limewekwa kwa watoto hasa wa kike na hivyo
kupunguza muda wa kujifunza na kupumzika pia ukosefu wa chakula
unaosababishwa na majanga ya tabia ya nchi kama ukame na mafuriko
inatufanya kushindwa kukaa shuleni kwa utulivu kujisomea na badala yake
tunashiriki katika shughuli za nyumbani za kutafuta kipato ambapo wazazi
wengine huozesha watoto wa kike ili kupata mali na kupunguza mzigo wa
malezi"amesema Sadiki.
Hata
hivyo baraza hilo la watoto wa manispaa ya Kinondoni kupitia Makamu
mwenyekiti wake,Saraphyner Frank limemkumbusha Rais Samia Suluhu
Hassan,wadau na serikali kwa ujumla kuwashirikisha watoto upangaji wa
bajeti,utungaji wa sera na mipango ya serikali kwa ujumla ili watoto
waone nao wana umuhimu katika mambo yanayohusu ustawi na makuzi yao hapa
nchini.
Maadhimisho ya
kimataifa ya siku ya watoto duniani yenye kauli mbiu isemayo "Ushiriki
na usawa kwa kila mtoto" yanafanyika kesho ulimwenguni kote ambapo
shirika la Save the Childrens Tanzania linaamini kuwa kama serikali
itaharakisha marekebisho ya sheria ya ndoa hatua hiyo itachochea watoto
wa kike kuwa salama,pamoja na kupitia sheria ya elimu na kanuni zake
ikiwemo kuondoa adhabu kali mashuleni kwa kutafuta njia nyingine mbadala
za kuendeleza nidhamu mashuleni,shirika hilo litakuwa tayari kusimamia
jambo hilo la uondolewaji wa adhabu kali mashuleni kwa kutoa mafunzo.


Comments