MFUMO WA UMILIKISHWAJI FUKWE KUPITIWA UPYA ILI KURAHISISHA UWEKEZAJI WA MAENEO YA FUKWE

 

MFUMO WA UMILIKISHWAJI FUKWE KUPITIWA UPYA ILI KURAHISISHA UWEKEZAJI WA MAENEO YA FUKWE




.......................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)  amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imependekeza kupitiwa upya kwa mfumo wa umilikishwaji wa fukwe ili kurahisisha mazingira ya uwekezaji na usimamizi wa maeneo ya fukwe nchini kwa lengo la kukuza utalii wa fukwe.

Ameyasema hayo leo jijini Mwanza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Nane la Maendeleo endelevu lenye dhima ya usimamizi madhubuti wa fukwe kwa maendeleo endelevu.

“Tunapendekeza mfumo wa umilikishwaji fukwe upitiwe upya ili ikiwezekana umiliki uhamishiwe katika wizara mojawapo kama Wizara ya Uwekezaji au Sekta ya Utalii kurahisisha uwekezaji na kutengeneza mazingira bora zaidi ya fukwe hizo” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amefafanua kuwa pendekezo hilo linatokana na maoni ya kikosi kazi kilichoundwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kilichopitia fukwe hizo na kugundua kuwa asilimia kubwa ya fukwe  zinamilikiwa na watu  binafsi lakini nyingine zinamilikiwa na Serikali za mitaa, hivyo kupelekea kutokuwa na uelewa wa pamoja juu ya uwekezaji katika maeneo ya fukwe.

Amesema changamoto hiyo inaweza kutatuliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi  ili kuweka uelewa wa pamoja juu ya uwekezaji katika maeneo ya fukwe na kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kuweza kuzifikia fukwe hizo kwa urahisi.

Aidha, amesema kikosi kazi hicho kilichoundwa mwaka 2016 kilitembelea mikoa kadhaa ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Tanga ,Mtwara na Lindi kwa lengo la kuzitambua na kuziainisha fukwe zilizopo katika maeneo hayo  na hatimaye kuleta mapendekezo ya kuzitambua fukwe na kuangalia umiliki wake sambamba na kuangalia jiografia zinazofaa kama zinawiana na masuala ya utalii.

Comments