HAYA HAPA MAFANIKIO YA ACT WAZALENDO KATIKA KUISIMAMIA SERIKALI KUPITIA "WASEMAJI WA KISEKTA

 HAYA HAPA MAFANIKIO YA ACT WAZALENDO KATIKA KUISIMAMIA SERIKALI KUPITIA "WASEMAJI WA KISEKTA, 2022



Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT Wazalendo Doroth Semu akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam.

CHAMA cha ACT Wazalendo kimetaja mafanikio kiliyoyapata tangu kuundwa kwa Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta miezi 10 iliyopita.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 28, 2022 jijini Dar es Salaam Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo Doroth Semu amesema kwa muda wa miezi 10 wamefanikiwa kutoa matamko rasmi ya kiuchambuzi yapatayo 95 na Mkutano na Waandishi wa habari 31 na ziara za wasemaji wa kisekta (Mawaziri Vivuli) saba.

“Ziara ya Waziri Mkuu Kivuli kwenye vyombo vya Habari; Ziara ya Mawaziri Vivuli wa Kilimo, Biashara na Nishati kwenye Mikoa ya Kusini, Ziara ya Waziri Kivuli wa Madini kutembelea Wachimbaji wadogo Geita; ziara ya Waziri Kivuli wa Biashara na Viwanda kutembelea ajali ya moto Soko la Karume; Ziara ya Waziri Kivuli wa Maji na Mazingira kufuatilia maendeleo ya Mradi wa visima vya maji Kimbiji na Kigamboni; Ziara ya Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Makazi katika kata ya Bunju na Wazo,” amesema Semu.

Semu akibainisha mafanikio hayo amesema kutokana na kupanda kwa gharama za maisha kutokana na bidhaa mbalimbali kupanda bei walitoa msimamo na mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuleta unafuu kwa wananchi. 

Kwamba walitoa pendekezo la kupunguza tozo, ushuru na kodi kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ambazo ni muhimu kwa maisha ya watu kama vile mafuta ya kula, sukari, ngano na mafuta ya petroli na diseli, na kuongeza uzalishaji wa chakula na mahitaji muhimu kwa nchi huku wakiitaka Serikali kuongeza umakini wa kudhibiti soko holela la nje (usafirishaji wa chakula nje) kwa ajili ya kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa za chakula.

Licha ya hapa na pale Serikali ilitekeleza baadhi ya mapendekezo tuliyowahi kutoa japo sio kwa ufanisi na kwa usahihi kama vile ilitoa ruzuku ya mafuta na mbolea, kuondoa kodi kwenye mafuta ya kula na kupunguza tozo za miamala ya kieletroniki (Simu na Benki),” ameeleza Semu.

Hata hivyo ameeleza kwamba mwenendo wa mfumuko wa bei (gharama za maisha) bado unazidi kupaa, hivyo, ameitaka Serikali kuweka mikakati ya kuhami maisha ya watu na kujiandaa kukabiliana na hali hiyo na kuwaandaa wananchi kuongeza uzalishaji na angalau kukidhi mahitaji ya ndani.

Kuhusu Miswada ya Sheria na kanuni zilizoenda Bungeni, amesema kupitia Kamati ya Wasemaji wa kisekta ya kuisimamia Serikali walifuatilia, kuchambua, kukosoa na kutoa mapendekezo kuhusu miswada kadhaa iliyowasilishwa.

Miongoni mwa miswada hiyo ni Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ambao uliwasilishwa na Serikali kwa mara ya kwanza bungeni Septemba 2022.

Kwamba pamoja na nia njema ya Serikali ya kutaka kupanua wigo wa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi kuingizwa kwenye mifumo ya bima, maudhui ya muswada huo yalikuwa na mapungufu mengi. 

“Tatizo tuliloliona ni kuwa sehemu ya wananchi walio sekta isiyo rasmi wasingeweza kumudu gharama za bima hiyo kutokana na viwango vya juu vilivyowekwa. Pia kiuchambuzi na uhalisia muswada ulikuwa unaimarisha na kukuza madaraja ya kupata huduma bora kama ilivyo sasa, kwa wasio na uwezo na wenye uwezo,” amesema Semu na kuongeza,
Pia, mfumo wa uchangiaji kutokuwa na uhakika na endelevu, uliwekeza kwenye kutumia mabavu kwa kuzuia watu kupata huduma zingine kama njia ya kuwavutia wananchi kujiunga na Bima ya Afya,”.

Hivyo amebainisha, ACT Wazalendo kwa kutambua changamoto ya afya, hususani gharama za matibabu zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi wengi.

Kutokana na umaskini, wengine hawana kipato cha uhakika kinachoweza kuwahakikishia wanapokuwa na magonjwa kumudu gharama hizo, wachache (ambao ni watumishi wa Serikali na wengine kwenye Sekta binafsi rasmi) ndio wenyewe uhakika wa matibabu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa au bima zingine.

Kwamba wananchi wengi wanatumia fedha kutoka mifukoni mwao wanapougua au kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHIF).

Amesema, waliupinga Muswada huo kwa sababu ulikuwa hauendi kuondoa matatizo ya msingi kwenye upatikanaji wa huduma bora za afya kwa usawa na kwa uhakika. 

“Tuliwaeleza tatizo la afya ya Watanzania halitokani na kukosa matibabu tu bali ni mazingira hatarishi ya kazi, watu kukosa vipato vya kueleweka, masikini kuendelea kuwa maskini zaidi, wazee kutopatiwa mahitaji yao ya msingi, umaskini wa chakula na kipato,” amebainisha Semu na kusema, 

“Mfumo utakaoimarisha afya ya watanzania na kuwezesha kugharamia matibabu kwa watu wote nchini ndio jawabu la kuimarisha afya na kukabiliana na changamoto za gharama za matibau. Sisi tulipendekeza mfumo wa hifadhi ya jamii kwa watu wote ambao ndani yake ungetoa fao la bima ya afya watu wote,”.

“Hatimaye Muswada uliondolewa rasmi Bungeni, tunatumai sasa kama wadau tutasikilizana ili kuboresha zaidi,”.

Kuhusu Kanuni ya Kikotoo cha Mafao ya Uzeeni, amesema Serikali ilirejesha kanuni hiyo iliyopigiwa kelele mwaka 2019 na kuifanyia marekebisho madogo.

“Kiukweli, ACT Wazalendo tulipambana kuhakikisha kanuni hizo zisipitishwe na Bunge kwa kutoa mapendekezo mbadala kupitia Kamati hii ya wasemaji wa kisekta,” ameeleza Semu.

Amesema uamuzi wa Serikali kutangaza Kanuni mpya uliweka kikotoo cha 1/580 badala ya 1540, pia malipo ya mkupuo ya mafao (kiinua mgongo) ya mtumishi aliyestaafu atalipwa kwa asilimia 33 badala ya 50% iliyokuwa inatumika kabla, umri wa kuhudumiwa mstaafu ni miaka 12.5 badala ya miaka 15.5.

Kwamba walionesha uchambuzi wa athari za kutumia kikotoo kipya chenye marekebisho madogo tu ya asilimia kutoka 25 hadi 33 na kuacha maeneo mengine kama yaliyovyo, namna yatakavyoenda kumpunja mstaafu. 

“Kutokana na matatizo ya kanuni za mafao tulizipinga kanuni hizi, kwa kuwa tunaamini Mfumo wa Hifadhi ya Jamii unapaswa kusaidia kulinda maisha ya watu na kutoa uhakika wa kuishi vizuri unapokutwa na majanga au kupoteza uwezo wa kufanya kazi kwa namna yoyote ile,”.

Kuhusu Muswada wa huduma za Habari amesema waliungana na wanahabari kupaza sauti kuhakikisha muswada huu unarekebishwa kwamba kazi hiyo wataendelea nayo mwaka 2023.

Comments