TUZO ZA MUZIKI WA REGGAE KUTOLEWA JANUARY 1,JIJINI DAR, WAZIRI MCHENGERWA KUWA MGENI RASMI.

 TUZO ZA MUZIKI WA REGGAE KUTOLEWA JANUARY 1,JIJINI DAR, WAZIRI MCHENGERWA KUWA MGENI RASMI. 



Na Mwandishi wetu, Dar es salaam

Tuzo za pili za muziki wa reggae na dancehall zinatarajiwà kutolewa januari mosi, 2023 Kwa wasanii na vikundi mbalimbali vya muziki huo.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, mratibu wa taasisi ya kiutamaduni ya Kukaye Moto Culture Center Dimateo Zion,mbao ndiyo waandaaji wa tuzo hizo amesema tuzo hizo zimelenga kutoa motisha Kwa wasanii wa muziki wa reggae na dancehall na kuwapa hamasa ya kuendelea kufanya kazi nzuri, kuupa muziki huo Kwa kufungua fursa za udhamini na wasanii kuweza kufanya kazi Kwa pamoja. 

Amesema Kwa mwaka huu wamefanya maboresho makubwa katika tuzo hizo tofauti na zile walizozitoa katika msimu wake wa kwanza mwaka 2020 ambapo pia vipengele zaidi ya 20 vitashindaniwa.

Ameongeza kuwa muundo wa kuwapata washindi wa tuzo hizo, kamati ya maandalizi inashirikisha watangazaji wa redio zenye vipindi vya reggae ambapo wasikilizaji watapewa fursa ya kutuma ujumbe mfupi wa maandishi na kipiga simu ili kuchagua washindi kwenye vipengele mbalimbali.

Aidha Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya maandalizi ya tuzo hizo za Kukaye Moto, Awards zinazofanyika hapa nchini Kwa msimu wa pili Bi Stella Kisinga amewataka wasanii wa muziki wa reggae na dancehall kuendelea kutoa nyimbo nzuri na kuendelea kuuheshimisha muziki huo na kuongeza kuwa tuzo hizo ni hatua kubwa ya heshima Kwa muziki wa reggae nchini.

Naye Afisa habari wa tuzo hizo ambaye pia ni mtangazaji wa vipindi vya reggae kupitia kituo Cha redio Cha Kiss FM Jijini Dar es salaam, Mussa Khalid ameviasa vyombo vya habari nchini hususan vituo vya redio na televisheni kuendelea kutoa sapoti Kwa muziki wa reggae na dancehall ili wanamuziki wa aina hiyo ya muziki wafurahie matunda ya kazi zao wanazofanya.

Miongoni mwa vipengele vitakavyoshindaniwa katika tuzo za Kukaye Moto Awards 2022 ni pamoja na Mtayarishaji bora wa nyimbo ya mwaka, video bora ya mwaka, muongozaji bora wa video wa mwaka, mwanamuziki bora wa kiume/kike wa mwaka, mwanamuziki bora chipukizi wa mwaka kiume/kike, wimbo bora wa kushirikiana wa mwaka pamoja na mtumbuizaji bora wa mwaka(reggae/dancehall)

Vipengele vingine ni pamoja na tuzo ya bend bora ya mwaka, kundi bora la mwaka, selekta (Dj)bora wa mwaka pamoja na Mwandishi bora wa mashairi wa mwaka (reggae/dancehall)

Tuzo za Kukaye Moto Awards zinatarajiwa kufanyika January 1,2023 katika hoteli ya Best Point iliyopo Ubungo, riverside Jijini Dar es salaam ambapo mgeni rasmi katika hafla ya utolewaji wa tuzo hizo anatarajiwa kuwa ni waziri wa Sanaa, utamaduni na michezo, Mhe Mohhamed Mchengerwa 

Comments