BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA LATANGAZA MAAZIMIO YAKE, LAMPONGEZA RAIS SAMIA KUONDOA ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA

 

BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA LATANGAZA  MAAZIMIO YAKE, LAMPONGEZA RAIS SAMIA KUONDOA ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA

   

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar ea Salaam.



BARAZA Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF) limepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuondoa zuio haramu la Mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa.

Hayo yamebainishwa leo Januari 26, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa CUF Taifa Profesa Ibrahim Lipimba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ya kikao chake cha Januari 21 hadi 22 mwaka huu.

Prof. Lipumba ameeza kwamba Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuwa “Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.”

“Aidha, Ibara ya 11(1)(a) ya Sheria ya Vyama vya Siasa inavipa haki Vyama vya Siasa kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima. Rais hana mamlaka ya kuzuia mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa. Tunampongeza Dr Samia kwa kutambua hili na kuacha kuendelea kuivunja Katiba ya nchi na sheria ya Vyama vya Siasa,” ameongeza Prof. Lipumba.

Kwamba Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeupongeza Uongozi wa Chama hicho Wilaya ya Ubungo kwa kufanya Mkutano wa Hadhara Januari 7, 2023 katika eneo la Manzese, Wilaya ya Ubungo.

Amebainisha kuwa mkutano huo ulifanyika siku ya nne baada ya kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa, na CUF kuwa Chama cha kwanza kufanya mkutano wa hadhara. 

Aidha amesema Baraza Kuu limewaelekeza wajumbe wote wa Baraza Kuu, viongozi na wanachama wa ngazi mbali mbali kuendelea kufanya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yao, kuelezea na kueneza sera za CUF za Haki Sawa na Furaha kwa Wananchi.

Akizungumzia kuhusu ubunge wa Afrika Mashariki, ameeleza kuwa Baraza Kuu limempongeza kwa dhati Wakili Msomi Mashaka Ngole kwa kuchagualiwa kuwa Mbunge wa Afrika Mashariki katika Uchaguzi uliofanyika Septemba 22, 2022.

Kwamba Baraza Kuu limemuagiza Mashaka Ngole awe Mbunge mahiri wa mfano katika kutetea maslahi ya Watanzania ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kuhusu taarifa ya kikosikazi Prof. Lipumba amesema Baraza Kuu limesikitishwa na muda mrefu uliotumiwa na Kikosikazi kilichoundwa chini ya ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuatia mkutano baina ya Msajili na Vyama vya Siasa na wadau wengine wa demokrasia, kukamilisha taarifa yake iliyowasilishwa kwa Rais Oktoba 21, 2022.
 
“Kikosi kazi kimetumia zaidi ya miezi 10 kwa ajili ya zoezi hilo. Kwenye Mkutano uliofanyika tarehe 15-17 Desemba 2021 jijini Dodoma, mambo yote ya msingi yalijadiliwa na kuanishwa. Mwezi mmoja ulitosha kabisa kwa Kikosikazi kidogo kuandaa taarifa ili Serikali iifanyie kazi kabla ya kupitisha bajeti yake ya 2022/23; ili yale yaliyokubaliwa yaanze kutekelezwa,” amebainisha Prof. Lipumba.

Comments