HAKI ELIMU YALAANI VIKALI ‘ADHABU YA VIBOKO” VIDEO YA MWALIMU MKUU AKICHARAZA BAKORA WANAFUNZI 2 KAGERA,YATOA MAPENDEKEZO 9 KWA SERIKALI.

 HAKI ELIMU YALAANI VIKALI ‘ADHABU YA VIBOKO” VIDEO YA  MWALIMU MKUU AKICHARAZA BAKORA WANAFUNZI 2 KAGERA,YATOA MAPENDEKEZO 9 KWA SERIKALI.


Na Thadei Praygod,Dar es salaam 

Shirika lisilo la kiserikali la HAKI ELIMU limelaani vikali tukio la adhabu ya kikatili waliyoipata wanafunzi wawili wa shule ya msingi Majanja wilayani Kyerwa mkoani Kagera kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo.


Hatua ya shirika hilo inafuatia kusambaa kwa video fupi katika mitandao mbalimbali ya kijamii nchini ikimwonysha mkuu huyo wa shule Isaya Benjamin akiwacharaza bakora kwenye nyayo za miguu wanafunzi wawili.


Akizungumza na waandishi wa habari leo januari 26,2023 mkurugenzi mtendaji wa shirika la Haki elimu,Dkt John Kalage amesema kuwa kitendo hicho kinakiuka siyo tu haki za watoto bali pia ni kinyume na maadili ya kazi ya ualimu na malezi bora kwa wanafunzi.


Dkt Kalage ameongeza kuwa shirika hilo linaipongeza serikali kupitia waziri wa elimu,sayansi na teknolojia Prof Adolf Mkenda na uongozi wa mkoa wa Kagera kwa kuchukua hatua za haraka na za awali dhidi ya mwalimu aliyehusika na ukatili huo ikiwa ni pamoja na kumvua nafasi yake ya ualimu mkuu,kumsimamisha kazi na kuunda tume ya kuchunguza tukio hilo ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.


Aidha Dkt Kalage ameongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya hali ya ukatili nchini iliyotolewa na jeshi la polisi,visa vya ukatili kwa watoto viliongezeka kwa asilimia 25.9% kutoka visa 5,803 vilivyoripotiwa mwaka 2015 hadi visa 7,388 mwaka 2020.


“katika utafiti uliofanywa na shirika la Haki elimu mwaka 2020,takribani asilimia 87.9 ya watoto wa shule waliripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 90 kati ya hao walisema ukatili wa kimwili waliofanyiwa ulitokana na adhabu za viboko zinazotolewa shuleni,huku asilimia 54.9 ya watoto walisema walimu wao na walezi wanatumia kupiga ngumi na makofi kama Sehemu ya adhabu’alisema Dkt Kalage.


Kutokana na matukio hayo shirika hilo pia limeishauri serikali kuchukua hatua ambazo zitakomesha kabisa matumizi ya adhabu za viboko shuleni na kuhimiza adhabu chaya/mbadala ambazo siyo za kikatili.


“ni rai yetu vipengele vya sheria ya elimu ya mwaka 1978,mwongozo wa elimu  juu ya adhabu za viboko wa mwaka 2002 na sheria ya mtoto ya mwaka 2009,vipitiwe upya ili kukataza kabisa matumizi ya viboko shuleni na kuzuia adhabu nyingine ambazo zinaweza kutoa mwanya wa ukatili wa watoto kufanyika”aliongeza Dkt Kalage.


Sambamba na hayo shirika hilo limetoa mapendekezo 9 kwa serikali ikiwa ni pamoja na program ya uanzishwaji wa shule salama 600 nchi nzima ambayo inalenga kuondoa ukatili wa namna yoyote na kuzifanya shule kuwa Sehemu salama na rafiki pa kujifunzia ambayo imetangazwa hivi karibuni na serikali,ilenge shule zote 18,000 nchini ikiwemo shule za msingi 12,000 na sekondari 5000.


Mapendekezo mengine yaliyotolewa ni pamoja na serikali kuweka mipango endelevu ya kuimarisha mifumo rasmi ya ulinzi na usalama kwa watoto ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa madawati ya ulinzi na usalama kwa watoto shuleni pamoja na wadau kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi,wazazi na jamii ili kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto katika maeneo ya shule,nyumbani,nyumba za ibada na maeneo yote ambayo watoto hukusanyika.


Hata hivyo Dkt Kalage ameongeza kuwa,Haki elimu inapendekeza serikali kuchukua hatua dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na vitendo vya ukatili wa dhidi ya watoto ili kuvikomesha ndani na nje ya shule pamoja na kuhuisha miiko na maadili ya walimu ili kuwagusa hata walimu ambao wanashindwa kuzuia matendo ya ukatili kwa watoto yanayofanywa na walimu wenzao mashuleni kama ambavyo imeonekana katika video ya tukio la mwalimu mkuu kupitia video iliyosambaa mitandaoni.

Comments