MOI KUANZA KUFANYA UPASUAJI WA KISASA WA UBONGO
MOI KUANZA KUFANYA UPASUAJI WA KISASA WA UBONGO.


Na Mwandishi wetu, Dar es salaam
Katika kuhakikisha inaendana na Kasi ya utoaji wa huduma bora za Afya zinazoendana na usasa wa sekta hiyo duniani hasa katika upande wa upasuaji TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), imeanza kutoa mafunzo ya mwaka mmoja kwa wataalmu wake, ambapo wagonjwa 40 watafanyiwa upasuaji wa kisasa wa kutoa damu iliyovuja katika ubongo na kuziba mishipa.
Hayo yametanabaishwa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo ,Dk Respisius Boniface alipokuwa Akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema wanapata ongezeko la wagonjwa waliopasuka mishipa ya damu kwenye ubongo na visababishi mbalimbali hasa presha.
Aidha Dkt Boniface ameviambia vyombo vya habari kuwa Kwa wiki taasisi hiyo hupokea wagonjwa waliopasuka mishipa ya damu kichwani na damu kuvuja katika ubongo saba mpaka 10 ambapo Kwa mwaka inakadiriwa kupata wagonjwa hao kwa 120 hadi 150.
Amesema watanzania wanapaswa kibali style ya maisha ambayo haitawapelekea kupata magonjwa kama hayo ambayo siyo ya kuambukiza na yamekuwa yakiwakumba watu wengi kutokana na staili zao za maisha
“Tumeona pamoja na kuzuia tujipange kuwatibu na tumeanzisha mafunzo maalum, ili kusaidia nchi yetu tutakuwa tunafundisha na tumeanza na Prof Atanasi kutoka Ujerumani haya ni mafunzo endelevu na Kwa sasa tumeanza na wataalamu wa MOI halafu baadae tutaenda na madaktari wa hospitali nyingine na tutafanya kwa mwaka mmoja,”amesisitiza.
Kuhusu gharama za uparesheni hizo Kwa hapa nchini Dk Boniface amesema oparesheni hizo zina gharama ya Sh milioni nane hadi 12 ambapo kama mgonjwa atafanyiwa upasuaji kama huo nje ya nchi itamgharimu shilingi milioni 50 hadi 60 hivyo kwa kila mgonjwa kiasi cha Sh milioni 40 zimeokolewa.
“Presha zamani ilikuwa watu wazima miaka 55 hadi 60, lakini sasa tunapata vijana hadi miaka 35 kwa sababu ya mabadiliko ya maisha na endapo mgonjwa akichelewa ubongo unakufa hata akifanyiwa matibabu hawezi kurudi kwenye hali ya kawaida,”ameeleza.
Kwa upande wake daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Nasforas Rutabasigwa amesema kuwa utaalamu unaongezeka, hivyo wanatarajia kufanyia wagonjwa 40 kwa mwaka na kwa awamu nne watawafanyia wagonjwa 10.


Comments