WAFANYABIASHARA ENEO LA KWA KIBADENI SINZA WAIOMBA SERIKALI, SAKATA LA KUTAKA KUONDOLEWA ENEO HILO

 

WAFANYABIASHARA ENEO LA KWA KIBADENI SINZA  WAIOMBA SERIKALI, SAKATA LA KUTAKA KUONDOLEWA ENEO HILO



23


Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka kituo cha polisi Urafiki Frank Nkusa akizungumza na wafanyabiashara hao.


Kibao kilichowekwa katika eneo hilo la wazi lililopo mtaa wa Mshori Kwa Kibadeni, Sinza Kwa Remmy likionyesha Kuanza Kwa mradi wa uboreshaji wa eneo hilo ambapo wafanyabiashara wanaofanya biashara zao hapo wamelalamika kutaka kuondolewa



Na Mwandishi wetu, Dar es salaam 

WAFANYABIASHARA wanaotaka kuvunjiwa maeneo yao ya biashara na kuondolewa katika eneo la Kwa kibadeni,Sinza B,kwa Remmy wameiomba Serikali ngazi za juu kuingilia kati sakata hilo ili kuwanusuru. 


Akizungumza mmoja wa wafanyabiashara hao Aswile Adamson amesema kwamba kabla ya kuhamishwa wangetakiwa kutengenezewa mazingira ya mahali pengine pakuhamia kwani kupitia biashara zao wanasomesha na kulipa kodi.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya uongozi wa Halmashauri ya manispaa ya Ubungo kuweka bango ambalo linaonyesha kuwa eneo hilo sasa kunajengwa bustani jambo ambalo wafanyabiashara hao wamepinga wakidai kuwa inataka kujengwa sehemu ya kuhifadhia na kuoshea magari. 

“Je tunaenda wapi, basi wangetutengenezea mazingira ya mahali pa kwenda kwani tunasomesha na kutoa kodi,” amesema Adamson na kuongeza,

“Tuombe Serikali itusaidie ngazi ya chini tunapata shida sana, tuombe Serikali ngazi ya juu itusaidie wananchi wake tunanyanyasika,”.

Wafanyabiashara hao wameendekea kuiomba serikali iangalie namna ya kuwasaidia ili wasiondoke eneo hilo kwani wanalitegemea katika shughuli zao za kujipatia kipato. 

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa Shina namba nane katika eneo hilo Maua Ramadhan amedai kwamba eneo hilo linataka kufanywa Garden (Bustani).

Hata hivyo amedai kwamba tangu mgogoro huo uanze hakuwahi kushirikishwa, lakini alishirikishwa siku wanataka kuweka kibao japo pia hakuhudhuria siku hiyo kwa sababu hakishirikishwa tangu mwanzo.

Amebainisha kwamba wafanyabiashara hao wapo muda mrefu tangu yeye ni msichana mdogo kwani walioanzisha wameshaondoka na wapo wengine.

Ameeleza kwamba kinachoonekana ni kuwa wanaotaka kuwaondoa hawajafuata utaratibu.

Naye Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Kituo kidogo Cha Polisi,Urafiki Frank Nkusa amewataka wafanyabiashara hao kuwa watulivu wakati jambo lao linatafutuwa ufumbuzi huku akiahidi kukutana na Afisa mipango miji wa Halmashauri ya Ubungo kwani Polisi hawapendi kuona kunatokea vitendo vya uvunjifu wa amani kupitia mgogoro huo. 

Amesema kwamba jambo hilo atalipeleka kwa afisa mipangomiji kwani lengo ni jambo limalizike kwa amani na mambo mengine yaendelee.

Comments