Mtoto Aliyezaliwa Katika Kifusi Cha Tetemeko la Ardhi Syria Apata Jina,Maelfu wajitokeza kumuasili.
Mtoto Aliyezaliwa Katika Kifusi Cha Tetemeko la Ardhi Syria Apata Jina,Maelfu wajitokeza kumuasili.

-Mtoto huyo aliokolewa huku kitovu chake kikiwa bado kimefungwa kwa mama yake aliyefariki katika mji wa Jenderis nchini Syria.
SYRIA: Mtoto wa kike, ambaye mama yake alifariki baada ya kujifungua chini ya kifusi cha nyumba yao nchini Syria baada ya tetemeko la ardhi Jumatatu, amepewa jina na makazi.
Mtoto huyo aliokolewa huku kitovu chake kikiwa bado kimefungwa kwa mama yake aliyekufa katika mji wa Jenderis nchini Syria. Baba yake na ndugu zake pia walikufa katika tetemeko hilo la ardhi.
Ameitwa Aya, ambalo linamaanisha 'muujiza' kwa Kiarabu.
Mjomba wa babake anasema atampeleka nyumbani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini kwa sababu wanafamilia wake wote wamefariki. Nyumba ya Salah al-Badran mwenyewe iliharibiwa na tetemeko la ardhi na kwa sasa anaishi kwenye hema na familia yake.
Video ya kuokolewa kwa Aya ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii. Kanda hiyo inaonyesha mwanamume akikimbia kutoka kwenye vifusi vya jengo la ghorofa nne lililoporomoka akiwa amemshika mtoto mdogo aliyefunikwa na vumbi.
Mwanamume wa pili alionekana kwenye video hiyo akiwa anakimbia kuelekea kwa mwanaume wa kwanza aliomuokoa mtoto huyo mchanga akiwa amebeba blanketi kukifunika kichanga hicho kutokana na halijoto ya chini ya sifuri huku wa tatu akilia gari limpeleke hospitalini.
Maelfu ya watu walikuwa wamejitolea kuasili mtoto huyo wa kike.
Mtoto huyo alilazwa katika hospitali kwa matibabu katika mji wa karibu wa Afrin. Alikuwa na matuta, michubuko, alikuwa baridi na anapumua kwa shida. Mke wa daktari amekuwa akimnyonyesha pamoja na mtoto wake.
Aya ni mmoja wa watoto kadhaa walioachwa yatima na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 siku ya Jumatatu.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limesema limekuwa likiwafuatilia watoto ambao wazazi wao wamepotea au kuuawa, na linashirikiana na hospitali kuwasaka wanafamilia ambao wanaweza kuwahudumia.


Comments