UWT NJOMBE WAMKEMEA MWANAMKE MWENZAO ALIYEMTELEKEZA MUME NA WATOTO KISA KUPOOZA.

 UWT NJOMBE WAMKEMEA MWANAMKE MWENZAO ALIYEMTELEKEZA MUME NA WATOTO KISA KUPOOZA



 UMOJA wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe umelaani vikali tukio la mwanamke mmoja mkoani humo Asha Kikondo kumtelekeza mumewe aitwaye Emilio Sanga pamoja na watoto wao watatu baada ya mumewe huyo kupatwa na tatizo la kupooza upande mmoja wa mwili wake.

Akizungumza walipomtembelea familia hiyo iliyopo Kata ya Ramadhani Mkoani humo, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe Scolastika Kevela amesema kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo ni cha kikatili huku akiiomba Serikali kupitia idara ya ustawi wa jamii kulishughulikia suala hilo.


Kwa mujibu wa mwanamme huyo, mkewe aliondoka nyumbani hapo akimuacha na watoto wanne wa kwanza akiwa na miaka 12 na wa mwisho akiwa na miaka mitatu baada ya kupata tatizo la kupooza upande mmoja wa mwili wake mwaka jana.


Amesema kutokana na kitendo hicho yeye na watoto wake wanaishi katika hali mbaya kiuchumi kutokana na kutokuwa na uwezo wa kufanya kazi yoyote kwa ajili kujipatia chakula na mahitaji mengine ya kimaisha kutokana na hali aliyonayo.


Akizungumzia hatua hiyo Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe Scolastika Kevela amesema kitendo kilichofanywa na mwanamke mwenzao huyo siyo tu cha kilatili bali pia kinaleta sifa mbaya kwa wanawake wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.


"Kama UWT Mkoa wa Njombe tunalaani kitendo hiki kwa nguvu zote, pengine huko wapo watu wanaofanyiwa ukatili kama huu, huyu ni mmoja tu ambaye UWT tumeibaini, ukweli tumehuzunishwa sana na tukio hili na zaidi tuwatake wanawake kubadirika" amesema Scolastika.


Amesema inashangaza kuona mwanamke huyo hajali hata watoto wake hao watatu ambao alibeba mimba zao miezi tisa na kuamua kuwakimbia huku akiwaacha bila msaada wowote akitambua kuwa mumewe ni mgonjwa.


Amewataka wanawake wenzake kuacha kuwa wakatili na badala yake wawe chanzo cha furaha na amani katika familia zao kwa kuwa kipekee waliumbwa kuwa faraja na siyo kuwa watu katili huku akiomba Serikali kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kusaidia familia hiyo.


Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Njombe Vicky Kihwelo amesema Ofisi yake inalifahamu suala hilo na tayari imeshaanza kuchukua kuona ni kwa namna gani wataweza kumsaidia.


Aidha ameitaka jamii hususani familia kuwa na upendo pale inapotokea mmoja kapatwa na tatizo lolote kama hilo ambao ameutaja kuwa ukatili wa kiuchumi.


Nao baadhi ya majirani wa familia hiyo wameiomba Serikali kumchukulia hatua mwanamke huyo kwani mbali na kutoroka nyumbani hapo pia amekuwa akifika nyumbani hapo na kumpiga mumewe huyo na kumpokonya chochote zikiwemo fedha ambazo mumewe huyo amekuwa akisaidiwa

Comments