ACT WAZALENDO YAAINISHA MASUALA MAKUBWA YALIYOIBULIWA NA WANANCHI KWENYE MIKUTANO YA HADHARA
ACT WAZALENDO YAAINISHA MASUALA MAKUBWA YALIYOIBULIWA NA WANANCHI KWENYE MIKUTANO YA HADHARA
Waziri Mkuu Kivuli wa Chama Cha ACT Wazalendo Dorothy Semu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeainisha masuala makubwa 10 yaliyoibuliwa na wananchi kwenye mikutano ya hadhara waliyofanya katika mikoa nane ya Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 26, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kivuli wa Chama hicho Dorothy Semu ameyataja masuala hayo kuwa ni kuhusu, hifadhi ya Jamii kwa wote, kupanda kwa Gharama za Maisha na mbolea kilio cha wakulima.
Masuala mengine ni TASAF na utumishaji Wazee na watu wenye ulemavu, Gesi Asilia Lindi kutowanufaisha wananchi, zao la Korosho mikoa ya Kusini mwa nchi, migogoro ya Ardhi, usalama wa wananchi, Tume Huru, Katiba Mpya na Mageuzi ya Kidemokrasia Nchini na Haki za Raia kwa Wananchi wa Kigoma.
Kuhusu hifadhi ya Jamii kwa Wote amesema “Tulipokuwa Tanga, msisitizo wetu mkubwa ulikuwa ni kuhakikisha watanzania wote wanakuwa kwenye utaratibu wa kujiandaa kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo magonjwa, uzee, ajali, majanga na hali ya kukosa ajira,”.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watanzania wamejiajiri mashambani, migodini, katika shughuli za uvuvi, ufugaji, au wapo kwenye sekta isiyo rasmi ambayo inachukua asilimia 86 ya nguvu kazi yote nchini,” ameongeza Semu.
Kwamba watu wote wasiokuwa kwenye ajira rasmi hawana mfumo mzuri wa kuwalinda na kuwahakikishia wanapata matibabu, pensheni, likizo au mapumziko ya uzazi wala kulindwa kutokana na majanga, fao la kukosa kazi (bei, majanga n.k) na hawana uwezo wa kuweka akiba kwa ajili ya baadaye.
Kwamba athari za haraka zinazolikumba kundi kubwa la watanzania kwa kutokuwepo kwenye mfumo wa Hifadhi ya Jamii utaiona kwenye suala la matibabu (upatikanaji wa huduma za afya). Kote tulikopita tumekutana na vilio vya wananchi kuhusu gharama kubwa za matibabu, kukosekana kwa huduma bora hususani kwa wananchi vijijini na maskini.
“Takwimu zinasaidia kuonyesha kukosekana kwa usawa katika utolewaji wa huduma za afya nchini. Ni watanzania Milioni 9 (9,094,624) pekee kati ya watu Milioni 61 ndio wana uhakika wa matibabu kupitia Bima ya afya, kati yao wenye uhakika zaidi ni wale wenye Bima ya afya ya Taifa (NHIF) na Bima Binafsi ambao ni wastani wa watu Milioni 4.8,” amesema Semu na kuongeza,
“Wote ni mashahidi kwa kiasi gani suala la gharama za afya (matibabu) zinavyowatumbukiza watanzaia wengi kwenye umaskini au namna linavyoongeza mzigo mzito watu maskini, watu wasio na vipato vya kueleweka (uhakika). Wataalamu wanaonyesha kuwa kila mtu mwenye kipato anatumia 10-25 ya shilingi mia anayopata katika kugharamia afya,”.
Hivyo amesema wito wao kwa wananchi ulikuwa ni kuwa Afya sio bidhaa kuuzwa kama shati sokoni mwenye nacho ndio anunue na asiyenacho aangamie.
Kwamba lazima Serikali ishiriki kuhudumia na kugharamia afya za watanzania kwa kutumia kodi na Ili kushiriki kikamilifu ni lazima Serikali kutunga upya sheria ya Hifadhi ya Jamii ili kila mtanzania awemo kwenye mfumo wa Hifadhi ya Jamii kupitia NSSF au PSSSF.
Soma kwa Undani na masuala mengine tisa yaliyoibuliwa na wananchi katika mikutano ya hadhara ya ACT Wazalendo
Mosi; Masikini wasiojiweza ambao ni milion 14 walipiwe na Serikali kwenye Hifadhi ya Jamii ili wapate; Bima ya afya; Mitaji ya kuanzisha shughuli za uzalishaji au biashara; Pensheni na fao la bei au majanga.
Pili; Kwa watu walio kwenye sekta isiyo rasmi kama vile wamachinga, wavuvi, wakulima, wachimbaji wadogo, wafugaji n.k wawezeshwe na Serikali (kwa kuchangia theluthi moja ambayo ni elfu 10) na wao kuchangia sehemu ya kipato chao (elfu 20) kuweka kwenye Hifadhi ya Jamii.
Tatu; Wafanyakazi walioajiriwa katika utumishi wa umma na sekta binafsi wataendelea kuchangia Hifadhi ya Jamii kwa utararibu wa sasa, lakini hawatokatwa tena sehemu ya mshahara wao tena kulipia Bima ya Afya. Michango yao katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii ndio itatoa Bima ya Afya kama fao. Hawatoendelea kukatwa mara mbili.
Kwetu, hatuhitaji tena matabaka ya watu wenye uhakika wa pensheni wanapostaafu na watu wasio na uhakika, hatutaki kuwa na watu wenye uhakika wa matibabu na wasio kuwa na uhakika. Ndio maana tunasema Hifadhi ya Jamii ya Wote kwa Maslahi ya Wote.
i. Kupanda kwa Gharama za Maisha
Kote tulikopita tumekutana na kilio cha wananchi juu ya ugumu wa maisha unaotokana na kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu kama vile chakula; mahitaji mengine kama sabuni, mafuta ya kula, vifaa vya ujenzi.
Tunaingia msimu wa pili wa kilimo huku tukishuhudia kupanda kwa gharama za maisha hususani bei za vyakula kama vile; Mchele- mwaka 2021 ulikuwa sh. 1500-2000 kwa kilo na bei ya sasa ni sh. 2900-4,000; Unga wa Ugali sh. 800-1000 (2021) kwa sasa sh. 1800-2200; Ngano sh. 1500-1800 (2021) kwa sasa sh. 2000-2500; Maharage sh. 1600-2000 (2021) kwa sasa sh. 3500-4000; Mafuta ya kula yapo maeneo kama vile Mtwara na Tunduru wananunua hadi sh. 8000 kwa lita.
Serikali inatafuta visingizo katika kukabiliana na bei za vyakula. Inataja vita vya Urusi na Ukraini. Inataja athari za Korona. Lakini kibaya zaidi wapo viongozi wanasema kuwa ni mwaka wa neema kwa wakulima.
Ukiutazama mnyonyoro wa thamani hatuwezi kuona mkulima mzalishaji akinufaika na bei za sasa kwa sababu wao walishauza tangu mapema baada ya mavuno. Mkulima gani anayeuza sasa hivi Mchele, Mahindi, Maharage n.k?
Serikali iache dhihaka. Suala la mfumuko wa bei na usalama wa chakula ni uhai na usalama wa taifa lolote. Hivyo, ni muhimu kuchukua hatua za haraka, za kati na muda mrefu. Katika kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka;
• Serikali iachie chakula chote kilichokuwepo kwenye ghala la Taifa na kufuatilia uuzaji wake kutoka kwa Wafanyabiashara.
• Pili, Chakula kilichosemwa na Serikali kwamba kimeingia nchini kisambazwe chote kwa haraka.
• Tatu, Serikali ijenge uwezo wa kuhifadhi chakula cha kutosha kupitia mradi wa Taifa (Mamlaka ya Uhifadhi wa Chakula-NFRA) na waanze kununua sasa.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments