WAZIRI VIWANDA NA BIASHARA ATAKA KIWANDA CHA VIUADUDU TBPL KIBAHA KUJITANGAZA

 WAZIRI VIWANDA NA BIASHARA ATAKA KIWANDA CHA VIUADUDU TBPL KIBAHA KUJITANGAZA



Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Ashatu Kijaji ameutaka uongozi wa Kiwanda cha serikali cha kuua viluwiluwi vya mbu TBPL kilichoko Kibaha mkani Pwani kuhakikisha kinajitangaza ndani na nje ya nchi ili kuongeza wigo wa masoko kwa kuuza bidhaa hiyo ya kipekee ambayo inazalishwa hapa nchini.

Dk. Kijaji ameyasema hayo kufuatia ziara maalum aliyoifanya ya kutembelea Kiwanda hicho na kushuhudia namna uzalishaji wa dawa za viuadudu unavyofanyika kiwandani hapo.

Akiwa kiwandani hapo Dk Kijaji licha ya kujionea namna uzalishaji wa bidhaa hiyo unavyofanyika amekitaka kiwanda hicho kuhakikisha kinajitangaza kwa nguvu zote ili kuweza kupata masoko ya ndani na nje ya nchi badala ya kutegemea soko la ndani ambalo kwa kiwango kikubwa limeonekana kuwa ni la kusuasua. 

“Ni Mwaka mmoja na miezi miwili tangu nimeteuliwa kuwa Waziri wa wizara hii kiukweli tunacho kiwanda ambacho serikali imetimiza wajibu wake wa kuwekeza ili kuondokana na suala la Maralia hapa nchini na wajibu wetu ni kuhakikisha tunatoa elimu ya kutosha juu ya matumizi ya dawa hii kwa ajili ya kuua viluwiluwi vya Maralia ili kutimiza adhima ya serikali na katika yote jitahidini kuhakikisha mnajitangaza ndani nan je ya nchi”. Alisitiza Dk Kijaji.

Katika kuanza na mpango huu Waziri Kijaji ameutaka uongozi wa kiwanda cha TBPL kuhakikisha unashirikiana na Mamlaka ya biashara hapa nchini TANTRADE katika kuhakikisha dawa hizo zinatangazwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa na mipango mikakati ya masoko itakayofanikisha elimu juu ya matumizi ya dawa hizo na faida zake kufika kwa watanzania wengi.

"NDC kwa kushirikiana na TBPL tunaendelea na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kimasoko ikiwemo kutumia mabalozi wetu walioko nje ya nchi pamoja na kuzishirikisha taasisi binafsi ikiwemo Doctors without Borders ambapo tayari wamekwisha chukua dawa kiwandani hapa”Alibainisha Mapunda.

Katika hatua nyingine Mapunda pia alibainisha juu ya nia ya kiwanda hicho kuanza rasmi uzalishaji wa viuatilifu vya mazao ili kuweza kupambana na wadudu waharibifu wa mazao ambapo dawa hizo mara baada ya kufanyiwa majaribio zimeonyesha mafanikio makubwa katika kupambana na wadudu hao ambao ni hatari kwa ustawi wa sekta ya kilimo hapa nchini.

Akibainisha mafanikio ya kiwanda hicho Mapunda, amesema kimesaidia kwa kiwango kikubwa katika kushusha kiwango cha Malaria hapa nchini mathalani visiwani Zanzibar ambapo kutokana na matumizi ya dawa hizo kiwango cha maambukizi ya Malaria kimeshuka ambapo hivi sasa kipo chini ya asilimia moja, pamoja na upatikanaji wa masoko ya nchi za nje mathalani katika nchi za Msumbiji,Niger,Eswatin pamoja na Angola

Kiwanda cha viuadudu cha TBPL kilichoko Kibaha mkoani Pwani ni kiwanda cha kipekee barani Afrika ambacho kinamilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kikiwa ni mahususi katika kupambana na Maralia nchini na kina uwezo wa kuzalisha kiasi cha lita milioni sita kwa mwaka ambapo ujenzi wa kiwanda hiki ni matokeo ya ushirikiano wa kidiplomasia baina ya serikali ya Tanzania na CUBA

Comments