ACT WAZALENDO YAITAKA SERIKALI KUIPA RUZUKU TAASISI YA MAFUNZO YA UANASHERIA KWA VITENDO,YASEMA GHARAMA KUBWA ZIMECHANGIA UFAULU HAFIFU (LST)
ACT WAZALENDO YAITAKA SERIKALI KUIPA RUZUKU TAASISI YA MAFUNZO YA UANASHERIA KWA VITENDO,YASEMA GHARAMA KUBWA ZIMECHANGIA UFAULU HAFIFU (LST)
NA MWANDISHI WETU.
Chama cha ACT WAZALENDO kimeitaka serikali kupitia wizara ya katiba na sheria itoe ruzuku kuwezesha taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo (Tanzania Law School-LST) ili kumudu gharama za uendeshaji kuliko kuruhusu gharama hizo kubebwa na wanafunzi hali inayopelekea wanafunzi hao kufeli mara kwa mara.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na waziri kivuli wa katiba na sheria wa chama hicho Victor Kweka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mpango wa bajeti wa wizara ya katiba na sheria kwa mwaka 2023/24.
Amesema mjadala mkubwa kuhusu taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo ulipata nguvu zaidi baada ya matokeo ya mitihani ya kundi la 33 Oktoba 5 mwaka 2022 ambayo yalionyesha ufaulu usioridhisha na baadaye kupandishwa kwa ada ya masomo katika taasisi hiyo.
“wizara ilichukua hatua za kuunda kamati iliyoongozwa na Dkt Mwakyembe ili kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko ya wanafunzi na wadau wengine juu ya ufaulu,kutokana na taarifa hiyo ya uchunguzi kuna changamoto ambazo tulitarajia zingetatuliwa ikiwemo upungufu na kukosa ubora kwa miundombinu ya kujifunzia,kutokuwepo kwa mahakama ya kujifunzia,madarasa kukosa vifaa vizuri,upungufu wa wakufunzi na watumishi pamoja na kutokuwepo kwa mgahawa wa chakula lakini hakuna hata moja lililofanyiwa kazi”alisema Kweka.
Alisema ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili taasisi hiyo ikiwemo ya masuala ya rufaa na utangazaji wa matokeo ya mitihani kwa mfumo wa kielektroniki ambazo zilihitaji kupangiwa bajeti kwa ajili ya kufanyiwa mapitio waziri aliahidi kulifanyia kazi lakini hata kwenye bajeti ya wizara iliyosomwa bungeni mpango wa kunusuru taasisi hiyo haukuwepo.
Kuhusu kupanda kwa ada Kweka alisema kuwa ada ya chuo cha sheria ilipanda kutoka shilingi milioni 1.5 mpaka Tshs milioni 2.9 kwa muda wa mwaka mmoja ambalo ni sawa na asilimia 88 ambapo pia malipo hayo yanapaswa kufanywa kwa mkupuo ili mwanafunzi aweze kupata vigezo vya kusajiliwa na kuendelea na kuendelea na masomo ya Sheria.
Alisema ongezeko hilo la ada kwa wanafunzi wa mafunzo ya uanasheria kwa vitendo linaongeza mzigo mzito kwao na kuwa kikwazo cha kupata elimu hiyo ambayo ni muhimu sana ambapo gharama kubwa za kupata elimu zinatengeneza matabaka ya upatikanaji wa elimu kati ya wenye nacho na wasio nacho.
“uamuzi huu ni kufanya elimu hii kwa vitendo ni biashara na siyo huduma,kwa hiyo wenye uwezo ndio wataweza kununua wasio na uwezo wataikosa”aliongeza Kweka.
Hata hivyo katika hatua nyingine chama hicho pia kimeishauri serikali kuangalia namna ya uandishi wa nyaraka za mahakama na matumizi ya sheria kwa kuuweka kwa kiswahili kwani kutokana na nyaraka hizo kuandikwa kwa lugha ya kiingereza imekuwa kikwazo kikubwa katika upatikanaji wa haki kwa watanzania wengi na hupelekea kuwepo kwa gharama kubwa za kutafsiri nyaraka hizo za kisheria.
Chama hicho kimeshauri kuwa ni vyema sasa wizara ya katiba na sheria kuimarishwa kwa matumizi ya lugha ya kiswahili katika kutoa huduma za kimahakama na kwenye uandishi wa nyaraka za kisheria hivyo jambo hilo linapaswa kuwekewa bajeti ya kutosha.



Comments