Skip to main content

Heri ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

 

Heri ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Jambo kubwa katika Maendeleo ya kisiasa miaka ya mwanzo ya UHURU ni MUUNGANO baina ya TANGANYIKA na ZANZIBAR uliofanyika siku kama ya leo mwaka 1964.

Muungano huu ulitokea baada ya mapinduzi ya ZANZIBAR na kutokamilika kwa majadiliano juu ya uundaji wa shirikisho la AFRIKA MASHARIKI yaliyoendeshwa toka Juni, mwaka 1963 hadi mwanzoni mwa mwaka 1964.

Tarehe 26 Aprili, mwaka 1964, Muungano uliasisiwa rasmi na Mwalimu Julius K. Nyerere, Rais wa Jamhuri ya TANGANYIKA, na Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa serikali ya Mapinduzi ya ZANZIBAR kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es salaam.

Waasisi hao walibadilishana nyaraka za Muungano.

Aidha, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alichanganya udongo wa TANGANYIKA na ZANZIBAR kuashiria Muungano wa nchi mbili kuwa moja, tukio ambalo lilishuhudiwa na Sheikh Abeid Amani Karume.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akawa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Sheikh Abeid Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama inavyoainishwa katika Hati ya Muungano ya mwaka 1964, Chimbuko la Muungano ni pamoja na udugu na uhusiano wa muda mrefu kati ya watu wa TANGANYIKA na ZANZIBAR, uhusiano wa kisiasa uliozaliwa katika harakati za kupigania Uhuru na dhana ya umajumui wa Afrika (Pan Africanism).

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Afrika, mataifa mawili yakawa yameungana kuwa Taifa moja.

Jambo hili lilionyesha kuwa hatua za kuelekea Umoja wa Afrika zinaweza kutekelezwa kisiasa kufuatana na dhamira ya wananchi na utashi wa viongozi wao.

Huu ndio Muungano pekee wa nchi mbili katika Bara la Afrika uliodumu muda mrefu na ni miongoni mwa michache iliyopo ULIMWENGUNI. CDE; MOHAMED MLUYA

Comments