MAJALIWA: WATANZANIA TUMIENI NISHATI MBADALA
****
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kubadilika na kutumia nishati mbadala ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumanne, Mei 30, 2023) baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya wiki ya Nishati inayofanyika katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Wizara ya Nishati inao wajibu wa kuendelea kutoa elimu juu ya matumizi sahihi wa nishati hiyo ikiwa ni utekelaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Serikali kupitia Wizara ya Nishati pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia imeunda kamati ya kitaifa inayoratibu utoaji elimu na kuonesha fursa za wajasiriamali ambao watahitaji kuingia kwenye sekta hii ya matumizi ya nishati mbadala.”
“Anzeni na taasisi za elimu majeshi, kambi za wakimbizi na kila mahali ambapo panakaliwa na watu zaidi ya mia moja nataka sasa maeneo hayo yawe anzilishi na tuachane na kukata miti. Tunataka watanzania waanze kutumia nishati mbadala, huu ndio muelekeo wa Taifa letu”
Pia ametoa rai kwa wajasiriamali waendelee kubuni na kutengeneza nishati mbadala kwa kutumia rasilimali mbalimbali zilizopo nchini ikiwemo vumbi la makaa ya mawe na mapumba za mahindi.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameupongeza Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwa kuendelea kuhakikisha wanaratibu mpango kupeleka umeme vijijini.
“Wale mliopewa jukumu la kusimamia hili, jiridhisheni na kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme, na muwasimamie wakandarasi ili wafanye kazi hiyo kikamilifu.”
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati Januari Makamba amesema wizara hiyo imejipanga kutumia makundi mbalimbali katika kuhamasisha Watanzania juu ya matumizi ya nishati mbadala. “Pamoja na hili Wizara fikapo Julai 2023 itazindua dira ya Nishati Safi ya kupikia”
Comments