Skip to main content

MAKADKT MPANGO AWATAKA VIONGOZI MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA KUZINGATIA MIPAKA NA MAJUKUMU YAO

 DKT MPANGO AWATAKA VIONGOZI MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA KUZINGATIA MIPAKA NA MAJUKUMU YAO


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala  za Mitaa  Tanzania (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha  Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) tarehe 29 Mei 2023.

Na Mwandishi Wetu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa viongozi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia mipaka na majukumu yao katika utendaji wa kazi ili kuepusha migogoro na miingiliano katika kuwahudumia wananchi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Amesema ni lazima watendaji na viongozi wote wa kisiasa kufanya kazi kwa pamoja na kufanya mazungumzo ya kujenga kwa manufaa ya wananchi panapotokea hoja au mitazamo tofauti katika utekelezaji.

Aidha Makamu wa Rais amewasihi viongozi hao kutambua lengo kuu katika nyadhifa zao ni kuwaletea wananchi maendeleo na siyo migogoro baina yao hivyo ni muhimu kuheshimiana, kuwajibika, kushirikiana kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuondoa vikwazo vyovyote vinavyoweza kukwamisha miradi hiyo. Pia amehimiza ushirikiano baina ya Madiwani na Wakurugenzi wa Halmashauri na kuondokana na tabia ya Madiwani kutoa maazimio dhidi ya Wakurugenzi pamoja Wakurugenzi kutowaheshimu Madiwani.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa Mapato na kudhibiti uvujaji wa mapato katika maeneo yao. Ametaja tathmini ya taarifa za mapato kutoka katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato yatokanayo na vyanzo vingine vilivyokusanywa kupitia mashine za POS imebaini katika baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa fedha hazipelekwi katika akaunti husika za benki hivyo amewasihi kuzingatia taratibu za fedha na kudhibiti matumizi yasiyo na tija.
 
Aidha amewahimiza Madiwani kusimamia vema Halmashauri zao na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato. Makamu wa Rais amemtaka Waziri wa TAMISEMI kuwachukulia hatua mara moja Viongozi na Watumishi wanaobainika kufanya matumizi mabaya ya fedha za umma, vitendo ambavyo husababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa kiwango cha chini kwa kuwa fedha zilizopangwa kwenda kwenye mradi husika huenda kwenye mifuko ya viongozi na watumishi wasio waaminifu.
 

Comments