Skip to main content

RC SERUKAMBA ATOA KONGOLE KWA RAIS DKT SAMIA KWA KUWAJALI WAKULIMA

 



NA MWANDISHI WETU

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wakulima nchini kwa kutoa mbolea za ruzuku.

Amesema kwa wakulima waliofanikiwa kutumia mbolea za ruzuku kwa msimu wa kilimo 2022/2023 wamenufaika na wameongeza uzalishaji.

"Wakulima waliotumia vizuri mbolea kwa kufuata ushauri wa maafisa ugani kwa zao la alizeti, mahindi na vitunguu mazao yapo vizuri  sana na wakulima watavuna vizuri" Serukamba alisisitiza. 

Mkuu wa Mkoa Serukamba ameeleza hayo tarehe 29 Mei, 2023 ofisini kwake alipokutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ruzuku ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Louis Kasera na Watumishi wa Mamlaka alioambatana nao wenye lengo la kuhamasisha  usajili na uhuishaji wa taarifa za wakulima kwa msimu ujao wa kilimo. 

Serukamba ameeleza kuwa, Mkoa wake umejipanga kuhakikisha usajili wa wakulima wote unafanyika kwa wakati na upatikanaji wa mbolea kwa msimu wa kilimo 2023/2024 unaimarika kwa kushirikisha wadau na wafanyabiashara wa mbolea ili wakulima waweze kunufaika na mbolea kwa wakati. 

Amesema, katika kutekeleza hilo yeye mwenyewe (Serukamba) atafanya vikao katika Wilaya zake na kukutana na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji, pamoja na viongozi ngazi ya kata na vijiji/mitaa ili kuhakikisha zoezi la usajili linafanyika kwa uhakika.

Akieleza lengo la kufika mkoani hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya ruzuku Louis Kasera alisema ni kuwahamasisha wakulima kujisajili kwa wakati ili ifikapo tarehe mosi Julai 2023 waweze kuanza kununua mbolea na kuzihifadhi na msimu wa kilimo utakapoanza mwezi Oktoba waweze kuzitumia  katika shughuli zao za kilimo.

Amesema, maandalizi ya mapema  yataepusha usumbufu wa kutumia muda mrefu kwenye foleni za kununua mbolea na wakati mwingine bila mafanikio. Ameongeza kuwa, Msimu ujao wa kilimo 2023/2024 Serikali imejipanga kuhakikisha maghala yatakayotumika kuuzia mbolea yanatambulika mapema na mawakala wanapatikana ikiwa ni pamoja na Vyama vya Ushirika ili wakulima wasipate hadha ya upatikanaji wa mbolea.

Ameeleza kuwa, usajili na uhuishaji wa taarifa kwa msimu ujao wa kilimo utawawezesha wakulima kupata mbolea kulingana na mahitaji ya zao kutokana na fomu kuongeza kipengele kinachomtaka mkulima kutaja aina ya mazao anayoyalima.

Naye Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati, Joshua Ng'ondya amesema tayari daftari za kuwasajili wakulima zimefika ngazi ya Mkoa na Halmashauri zao na kuwataka wakulima kujitokeza kwa wingi ili waweze kusajiliwa kwa wakati na wahudumiwe kwa wakati.

Comments