Skip to main content

Rais Samia amtaka Kamishna Wakulyamba kurejesha nidhamu ya jeshi la uhifadhi

 


Na John Mapepele 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan amemtaka Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Kamishna Benedict Wakulyamba kwenda kusimamia nidhamu 
ya Jeshi la Usimamizi wa Hifadhi ili kuboresha sekta ya Maliasili na Utalii.

Mhe. Rais Samia ametoa kauli hiyo mara baada ya kumaliza kumwapisha  Wakulyamba leo Juni 17, 2023 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Aidha, amesema pamoja na kazi hiyo  Wakulyamba  atapangiwa kazi nyingine na Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Mabalozi na Washauri wa Rais wamekula kiapo cha maadili katika utumishi wa Serikali.

Akiongea na Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mara baada ya kukaribishwa na Katibu Mkuu Dkt Hassan Abbasi, Kamishna  Wakulyamba amesema anashukuru kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa watumishi wa Wizara hiyo.

Aidha amesema anamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini katika nafasi hiyo ambapo amesisitiza kuwa atafanya kazi kwa weledi huku akiomba ushirikiano.

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo Anderson Mutatembwa ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) amewashukuru watumishi wa Maliasili kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi cha takribani miezi mitatu akiwa hapo.

Tayari Kamishna Wakulyamba ameanza kazi rasmi katika Ofisi yake mara baada ya kuapishwa leo na  kutoka katika viunga vya Ikulu ya  Chamwino jijini Dodoma

Comments