RAIS SAMIA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA KIMATAIFA DAWA ZA KULEVYA




Na  Mwandishi wetu, Dar es salaam 

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya kimataifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam na kamishna jenerali wa tume ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, Aretas Lyimo alipokuwa Akizungumza na waandishi wa Habari juu ya masuala mbalimbali ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambapo amesema lengo la maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia June 23-25 mwaka huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha ni kuongeza uelewa we jamii na kuhamasisha umma kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Amesema kuwa maadhimisho hayo yenye kauli mbiu isemayo "Tuzingatie utu na kuboresha huduma za kinga na tiba" yataambatana na maonyesho ya shughuli mbalimbali za udhibiti  zinazofanywa na mamlaka pamoja na wadau wake katika udhibiti wa dawa za kulevya na utoaji wa elimu Kuhusu dawa hizo.

Aidha katika hatua nyingine mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DCEA) Imeingia makubaliano na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, TAKUKURU yatakayofanikisha kutolewa Kwa elimu juu ya matumizi ya dawa za kulevya kupitia klabu Mbalimbali za kupinga rushwa mashuleni na vyuoni

Comments