SERIKALI YAOMBWA KUPITIA UPYA SHERIA YA KODI, USAFIRISHAJI MAFUTA NJE YA NCHI KWA MALORI

 SERIKALI YAOMBWA KUPITIA UPYA SHERIA YA KODI, USAFIRISHAJI MAFUTA NJE YA NCHI KWA MALORI




Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeombwa kurekebisha sheria zake za kodi katika usafirishaji wa mafuta nje ya nchi ili kuongeza idadi ya wafanyabiashara watakaotumia bandari ya Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mwinjilisti na mfanyabiashara Alphonce Temba amesema wasafirishaji wa mafuta nje ya nchi wamekuwa wakiumizwa na sheria hizo kwa kutozwa kodi hata pale inapotokea ajali na mafuta kumwagika.


Aidha amelalanikia kitendo cha mamlaka hiyo kuitoza kodi ya milioni 20 kampuni ya Mafuta ya Malawi ya RASHY Motors kutokana na lori yake kumwaga mafuta mara baada ya kupata ajali ya kugongwa kwa nyuma na lori lingine lililokuwa linaendesha na dereva Mtanzania katika eneo la Igawilo mkoani Mbeya.


Ameongeza kuwa hali hiyo inasababisha wafanyabiashara wengi kuikimbia bandari za Tanzania na kwenda za nchi jirani ikiwemo Msumbiji ambayo sheria zao ajali kama hiyo ikitokea wajibu wa mfanyabiashara ni kusafisha barabara na mafuta yaliyomwagika hayatozwi kodi huku Tanzania ikiyahesabu mafuta hayo kuwa yametumika nchini hivyo yalipiwe kodi.


“Wafanyabiashara wa Malawi wanapenda kupitisha mafuta yao hapa nchini kutokana na ubora wa barabara za Tanzania kuliko Msumbiji hivyo kama sheria za TRA hazitarekebishwa tutegemee wafanyabiashara wa nchi wakiendelea kupungua” Amesema Bw. Temba.


Hata hivyo amesisitiza serikali kuangalia upya suala hilo kwa kurekebisha sheria za TRA  kwani kuendelea kuzitumia kutawakimbiza wafanyabiashara na kuikoseha serikali mapato.

Comments