HEKARI 535 ZA MIRUNGI ZATEKETEZWA KILIMANJARO


HEKARI 535 ZA MIRUNGI ZATEKETEZWA KILIMANJARO


********

Katika kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomea nchini Mamlaka ya kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, imefanikiwa kuteketeza  hekari 535 za mashamba ya mirungi katika  operesheni maalum ya ‘‘Tokomeza Mirungi’’ iliyofanyika katika vijiji vya  Rikweni, Heikondi, Tae na Mahande vilivyopo katika kata ya Tae, wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Operesheni hii iliyolenga kukabiliana na kilimo cha mirungi imefanyika kwa siku saba mfululizo kuanzia tarehe 2 hadi 9 Julai, 2023 na jumla ya watuhumiwa tisa (09) wamekamatwa kuhusiana na uzalishaji, usafirishaji na biashara ya mirungi na  watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Operesehni hiyo imefanyika ikiwa ni siku chache baada ya Maadhimisho ya kupiga vita dawa za kulevya kufanyika  Arusha ambapo Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo  Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza jitihada zaidi ziongezwe katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini ili kuokoa jamii katika janga la dawa za kulevya.



Kamishna Jenerali DCEA, Aretas Lyimo amesema operesheni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Katika kukomesha kilimo cha dawa za kulevya hapa Nchini.

Amesema Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kilimo cha Mirungi na bangi kinatokomea.

 Operesheni hii ambayo umefanyika kwa muda wa siku nane ni  endelevu na itaenda sambamba na  utoaji wa elimu ili kujenga uelewa kwa jamii juu ya athari za mirungi na dawa nyingine za kulevya kwa  wakazi wa vijiji hivi. Pia elimu juu ya mazao mabadala pamoja na kuwawezesha kuzalisha mazao hayo. Hii itawafanya wananchi husika kuona fursa ya kulima mazao mengine na kuachana kabisa na kilimo cha mirungi,” amesema Jenerali Lyimo.

Baadhi ya wananchi katika vijiji hivyo vinavyolima mirungi wameiomba Serikali kutoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya hususani Mirungi na kuahidi kuwa  watafanya vikao  kuhamasishana kuhusu hatari ya kilimo hicho na kwa pamoja washirikiane kuyafyeka na kuyaondoa kabisa mashamba yote ya mirungi katika maeneo yao.


Aidha, baadhi ya viongozi wa dini katika kata ya Tae wameeleza kuwa, wataendela kutoa elimu juu ya madhara ya mirungi kwa waumini wao. Elisante Senkondo mkazi wa kijiji cha Rikweni  na mchungaji wa kanisa Assemblise of God amesema kuwa wako tayari kushirikiana na serikali  kutoa elimu hiyo.

" Naiomba  serikali ingupa nafasi tukae na watu wetu katika Makanisa tuendelee kuwashauri kwa nguvu zaidi ili kwa hiari  yao wenyewe waweze kukubali kutokomeza haya madawa ya kulevya" amesema Mchungaji Senkondo

Comments