KENYA YAJIFUNZA MAFANIKIO YA STAMICO,YASEMA IMEJIFUNZA MENGI SEKTA YA MADINI TANZANIA
Ufanisi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na Wizara ya Madini kwa ujumla waivutia Kenya na kuifanya kuja Tanzania kujifunza utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uchimbaji madini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Uchumi wa Bluu nchini Kenya Elijah Mwangi wakati wa ziara yake ya wiki moja akiambatana na ujumbe wa wataalamu sita kutoka nchini humo waliokuja kujifunza na kuona jinsi STAMICO na Wizara ya Madini kwa ujumla wanavyofanya shughuli zake .
Mwangi ameipongeza STAMICO na kusema kuwa imekuwa ikifanya vizuri katika kuendeleza shughuli za mnyororo wa thamani wa uchimbaji madini hivyo wataendelea kujifunza kwa namna ambavyo imefanikiwa katika kuendesha shughuli za madini zikiwemo utafiti, uchimbaji, uchakataji, na biashara ya madini
Amesema anaamini kuwa kwa sasa Tanzania inanufaika vya kutosha kutokana na rasilimali hizo kupitia sheria na taratibu zilizowekwa.
“Tumejifunza mambo mengi kwa jinsi gani madini yanaweza kubadilisha maisha ya wanajamii na Taifa kwa ujumla, tumekuja hapa ili kuweza kujifunza, kwa sababu sisi bado ni Shirika changa ambalo hatuwezi kujilinganisha na STAMICO ambalo limeanza muda mrefu, na hatukuona sababu ya kuchagua nchi nyingine kwaajili ya kujifunza isipokuwa Tanzania, tunashukuru sana kwa kuwa majirani wema na kufungua milango kwaajili yetu.” Amesema Mwangi.
Mkuu Wizara ya Madini na Uchumi wa Bluu nchini Kenya Elijah Mwangi |
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amefurahishwa na ujio wa ujumbe huo ambao umeona ni vyema kujifunza kutoka Tanzania juu ya shughuli za uchimbaji na usimamizi wa rasilimali madini, huku akiamini kuwa ushirikiano huo utasaidia kukuza diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo.
“Tumejadiliana mengi na tumebadilishana uzoefu wa namna ya kuendesha Sekta ya Madini, nini kinatakiwa kufanyika hasa kwenye maeneo ya masoko, kuwawezesha wachimbaji wadogo na usafishaji wa Madini ili kuhakikisha maslahi katika shughuli yoyote inayohusiana na utafutaji na uchimbaji wa madini inasaidia kuleta mabadiliko kwenye sekta ndogo ya uchimbaji sambamba sekta zingine
Comments