TASAC NA NBS KUZINDUA TAARIFA YA SENSA YA VYOMBO VIDOGO VYA USAFIRI MAJINI KESHO DAR.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la uwakala wa meli Tanzania,TASAC,Kaimu Abdi Mkeyenge 


NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM

Shirika la uwakala wa meli Tanzania (TASAC)kwa kushirikiana na Ofisi ya  takwimu ya Taifa (NBS)wanatarajia kuzindua taarifa ya sensa ya vyombo vidogo vya usafiri majini.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 10,2023 jijini Dar es salaam,Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Kaimu Abdi Mkeyenge amesema sensa hiyo iliyofanyika mwaka wa fedha 2021/2022 ilihusisha katika maeneo ya pwani za bahari ya Hindi,maziwa,mito na mabwawa katika eneo la Tanzania bara.

Amesema sensa hiyo ilihusisha kuandaa taarifa ya sensa yenyewe na kuundwa kwa kanzidata (database)ya vyombo vidogo vya usafiri majini na itakuwa msaada mkubwa kwa Taifa hususan sekta ya usafiri wa majini kwa vyombo vidogo.

Aidha ameongeza kuwa kanzidata iliyoundwa ina taarifa nyingi muhimu ikiwa ni pamoja na taarifa za vyombo zenyewe,umiliki wa vyombo,matumizi ya vifaa na visaidizi vya kuokolea maisha ,mahali vilipo vyombo vidogo vya usafiri majini,matumizi ya vyombo hivyo na nyenzo zinazotumika katika kuzuia uchafuzi wa mazingira majini ikiwemo nyenzo zinazotumiwa na wamiliki wa vyombo hivyo katika mawasiliano.

Hata hivyo Bw Mkeyenge amawataka wadau wote kushiriki katika uzinduzi wa taarifa hiyo ya sensa ambapo pia tukio hilo litarushwa mubashara na chaneli ya mtandao wa Youtube wa wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Hafla ya uzinduzi huo inatarajiwa kufanyika kesho Julai 11,Katika ukumbi wa mikutano wa Arnatouglu  jijini Dar es salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa naibu waziri,wizara ya ujenzi na uchukuzi,sekta ya uchukuzi Mheshimiwa Atupele Mwakibete

Comments