MWELI AWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI SOKO LA MBOLEA


****************

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gelard Mweli amewahakikishia ushirikiano na  uwepo wa soko la mbolea wawekezaji kutoka nchini Indonesia walioonesha nia kuwekeza kwenye kiwanda cha kuzalisha mbolea nchini.

Amesema, madhumuni ya serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbolea Afrika na kueleza kuwa, tasnia ya mbolea imepewa kipaumbele na serikali ili kuongeza mchango wa Sekta ya Kilimo kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 na kueleza uwekezaji huo utawezesha malengo ya serikali kufikiwa.

Mweli ametoa kauli hiyo leo tarehe 23 Agosti katika kikao baina ya Wizara yake na taasisi zinazosimamia tasnia ya mbolea ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kampuni la Mbolea Tanzania (TFC) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Mweli ameongeza kuwa, utayari wa serikali katika kukuza Sekta ya kilimo ni mkubwa na imeamua kuweka ruzuku kwenye mbolea ili kuongeza matumizi ya mbolea kwa wakulima huku akibainisha kuwa matumizi ya mbolea yameongezeka baada ya serikali kuanza kutoa ruzuku ukilinganisha na ilivyokuwa kabla ya serikali kutoa ruzuku.

Aidha, ameeleza uwepo wa mfumo wa kidigitali wa kusambaza mbolea kwa wakulima ukiwa na manufaa makubwa kwa serikali na wafanyabiashara na kueleza mfumo huo unasaidia katika shughuli nzima ya malipo ya ruzuku inayotolewa na serikali.

Akiwahakikishia uwepo wa soko, Katibu Mkuu Mweli ameeleza kuwa, Tanzania imezungukwa na nchi nane zinazotegemea kutumia bandari ya Dar esSalaam kufkishiwa mbolea, na kubainisha ujenzi wa kiwanda utatosheleza mahitaji ya ndani lakini pia itahudumia nchi Jirani zilizopakana na Tanzania.

Akiwasilisha andiko linaloonesha namna kampuni hilo la ESSA litakavyotekeleza ujenzi wa mradi wa kiwanda cha mbolea nchini Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni, Kanishk Laroya amesema jina la kampuni lao linamaanisha umoja na kueleza utambulisho wao unalenga katika nia ya kushirikiana na kuwa bora katika kila wanachokifanya katika uwekezaji wao huku wakitanguliza utu.

Ameongeza kuwa, Kampuni hiyo ina nia ya kuchangia mafanikio ya nchi yeyote wanakofanya kazi kwa nia moja na kuiomba Tanzania kuwaunga mkono ili waweze kufikia malengo ya ujenzi wa kiwanda cha mbolea kwa mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Akielezea namna wanavyoendesha viwanda vyao nchini Indonesia, Rahul Puri Mjumbe wa Bodi amesema, wao wanazalisha mahitaji yote ya viwanda vyao isipokuwa gesi pekee. 

Amesema, wanazalisha umeme, Amonia, maji na bidhaa nyingine zinaotumika kama malighafi katika viwanda vyao.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Dkt. Stephan Ngailo ameeleza kuwa juhudi za serikali za kuwekeza zaidi kwenye miradi ya umwagiliaji kutaongeza idadi ya wakulima na kiasi cha mbolea kitakachohitajika kutokana na uhakika wa kulima kwa misimu mitatu kwa mwaka mzima.

Ameongeza kuwa, kwa msimu wa kilimo 2022/2023 kiasi cha tani 560 za mbolea kilitumika na hii ni kwa sababu kuna baadhi ya maeneo ambayo hayakufikiwa na huduma hii na hali ya ukame ambapo ili kutatua changamoto hizo vyama vya ushirika vimesajiliwa ili kuwafikishia wakulima mbolea karibu na maeneo yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni la Mbolea Tanzania (TFC) Samuel Mshote amewahakikishia wawekezaji hao uwepo wa malighafi za viwanda vya mbolea kwa wingi nchini kama vile phosifeti na kueleza uwepo wa makaa ya mawe yanayoweza kutumika katika kuzalisha umeme.  

Mshote ameleza nia ya kampuni lake kushirikina na wawekezaji hao na kutaka ushirikiano kuimarika kutokana na kushirikina katika kusukuma maono ya serikali pamoja serikali kwa ujumla katika kukuza tasnia ya mbolea nchini.

Wajumbe wa kampuni hiyo ni miongoni mwa wajumbe walioambatanza na Rais wa Indonesia  Joko Widodo aliyekuwa na ziara ya siku mbili nchini tarehe 21 na 22 Agosti, 2022 kwa ziara ya kikazi.

Comments