Skip to main content

POLISI DAR YAKAMATA ASKARI WAKE,TUHUMA ZA MAUAJI YA WATU WAWILI

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
.

NA MWANDISHI WETU

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia na kuwahoji kwa kina askari wa kampuni ya ulinzi PASCO LTD  11, Maafisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS)  wawili na askari Polisi 6.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 29, 2023 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

“Kushikiliwa kwa watu hao kunatokana na tuhuma za kujeruhiwa kwa watu wawili ambao baadae walipoteza maisha na suala hili uchunguzi wake tayari unaendelea kufanyika,” amesema SACP Muliro.

SACP Muliro ameeleza kuwa Agosti 28, 2023 majira ya saa 8 (nane) usiku eneo la Kiluvya Ubungo, maafisa kutoka katika taasisi hizo wanadai wakati wa  utekelezaji wa majukumu yao, lilitokea kundi la watu wanaokadiriwa kuwa 30 wakiwa na pikipiki zilizokuwa zimebeba magunia ya mkaa ambayo ni mazao ya misitu na walipofika eneo la ukaguzi  na kuamriwa wasimame, walikaidi na kuanza  kufanya fujo kubwa  kwa kuwarushia mawe Maofisa wa maliasili na wenzao wakishinikiza pikipiki  zilizo kuwa na mkaa kinyume na sheria ziachiwe.

Kwamba Mafisa wa timu hiyo waliokuwa na silaha walianza kufyatua risasi kwa lengo la kuwatawanya na kujilinda.

Amesema hata hivyo ilibainika watu wawili walijeruhiwa katika purukushani hizo na walipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitali ya Mloganzila.

Kwamba katika tukio hilo Pikipiki 16 ambazo zilitelekezwa na watu hao na magunia ya mkaa vilipelekwa Mpingo House.

Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum linachunguza mazingira yote ya tukio hili kwa kushirikiana na mamlaka zingine za kisheria na halitasita kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua zingine za kisheria kulingana na sheria za Nchi. Watu waliokuwa kwenye kazi hiyo wako chini ya ulinzi na silaha zao zimepelekwa kwenye mamlaka za kiuchunguzi za silaha/bunduki Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mloganzila kwa uchunguzi.  

Comments