SHEIKH MWAIPOPO AWAJIA JUU DKT SLAA NA AKINA MDUDE,AWATAKA WASISINGIZIE BANDARI KATIKA KUKAMATWA KWAO
SHEIKH MWAIPOPO AWAJIA JUU DKT SLAA NA AKINA MDUDE,AWATAKA WASISINGIZIE BANDARI KATIKA KUKAMATWA KWAO
NA MWANDISHI WETU
KATIBU wa Baraza la Habari la Kiislamu (BAHAKITA) Sheikh Said Mwaipopo amesema kuwa Boniphace Mwabukusi, Mdude Nyagali pamoja na Dkt. Wilbroad Slaa wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.
Sheikh Mwaipopo amebainisha hayo leo Agosti 17, 2023 akizungumza na waandishi wa habari Jijini Des Salaam kufuatia Madai ya wanaharakati wa haki za binadamu kwamba wamekamatwa kwa kukosoa mkataba wa DP World.
Hivyo amesema kwamba wamekamatwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kutoa kauli za kuhamasisha uvunjifu wa amani.
"Dkt. Slaa na Mdude wametoa kauli za kuhamasisha uvunjifu wa amani, walisema wataiwajibisha na kuipindua serikali, viongozi ni wezi pamoja na kuvamia vituo vya Polisi na ofisi za CCM” amesema Sheikh Mwaipopo.
Sheikh Mwaipopo amesema kuwa kauli walizotoa wanasiasa hao inatosha Jeshi la Polisi nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.
Amesema kuwa nchi ya Tanzania ina vyombo vya sheria, ulinzi na usalama pamoja na Jeshi la Polisi ambalo miongoni mwa majukumu yake ni kukamata, kuhoji na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.
“Nimepata wasiwasi baadhi ya taasisi ambazo zinasimamia haki za binadamu wamasema sio haki kuwakamata, walivyosema wanavamia vituo vya Polisi na kuwakamata watu kuna mahusiano gani na masuala ya uwekezaji wa bandari ? ” amesema Sheikh Mwaipopo.
Amefafanua kuwa mkataba wa uwekezaji wa bandari hauna mahusiano yoyote na Jeshi la Polisi na CCM “Wanaojiita watetezi wa haki za binadamu, hizo haki zipo kwa waharifu tu, walitaka waachiwe ili wakachome moto vituo ya polisi na ofisi za CCM ?” amesema Sheikh Mwaipopo
“Hawa watu hawajakamatwa kwa sababu ya kupinga uwekezaji, wamekamatwa kwa maneno yao machafu ambayo hayavumiliki na serikali yoyote duniani”amesema Sheikh Mwaipopo.
Amesema kuwa serikali ipo sahihi kuwakamata kutokana na kauli zao, na kila mtanzania anayo haki wa kukemea vitendo ambavyo sio rafiki.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Mwabukusi na Mdude waliokamatwa Agosti 12 Mikumi Mkoani Morogoro na wanashikiliwa kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi, huku Dkt. Slaa aliyekamatwa Agosti 13 jijini Dar es Salaam akishikiliwa kwa tuhuma hizo.
- Get link
- X
- Other Apps



Comments