VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA KUPITIA TGNP VYAJIVUNIA MAFANIKIO,SASA KUENDELEA KUSAMBAA NCHINI KOTE


mratibu wa vituo vya taarifa na maarifa,TGNP Jacqueline Mtesha akitoa mada katika warsha hiyo


 Na PrayGod Thadei

Mwaka 2010 mtandao wa kijinsia hapa nchini TGNP ulianzisha vituo vya taarifa na maarifa kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kwa kuhakikisha changamoto hizo zinafika katika mamlaka husika na kupatiwa ufumbuzi

 Tangu wakati huo yapata Miaka 13 vituo hivyo vimeleta mafanikio makubwa kwa jamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kuipa jamii hususan wanawake sauti ya kusemea vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia na hata kupeleka maendeleo katika maeneo yaliyo nyuma katika nyanja mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara,shule na hata upatikanaji wa huduma za afya

 Huku mtandao huo ukiwa unatimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwezi oktoba mnamo mwaka 1993 ni wazi vituo vya taarifa na maarifa ni moja ya mambo ambayo unaweza kujivunia nayo.

 Akizungumza katika warsha ya siku moja kwa waandaaji na watangazaji wa vipindi vya redio pamoja na baadhi ya wenyeviti wa vituo vya taarifa na maarifa [knowledge Center] CK  iliyofanyika makao makuu ya mtandao huo yaliyopo Mabibo jijini Dar es salaam,mratibu wa vituo hivyo Jacqueline Mtesha amesema kuwa mpaka sasa kuna vituo 75 katika mikoa 15 hapa nchini na bado wanaamini vitaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

 Bi Mtesha ameongeza kuwa Vituo vya Taarifa na Maarifa, vimekua nguzo muhimu katika ujenzi wa vuguvugu la mabadiliko kwenye jamii hususani katika masuala ya usawa wa kijinsia na maendeleo amapo  Katika kuimarisha vituo hivyo; TGNP imekuwa ikiendesha mafunzo kwa makundi mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari ili kutoa elimu juu ya vituo hivyo na kazi zake ngazi ya jamii.

"Vituo hivi vya Taarifa na maarifa ni msaada mkubwa kwa jamii,katika kuepukana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wakiona/kusikia kitendo cha ukatili watahakikisha wanalivalia nyuga na kulifikisha katika ngaxi zote za kiserikali zinazo husika ili muhusika achukuliwe hatua kama anafungwa afungwe na kuhakikisha hata yule aliyekuwa anafanyiwa vitendo vya ukatili anakuwa sehemu salama".Amesema Mtesha

Aidha kwa upande wake mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa Kata ya  Saranga Bi Maria Mwigune amesema kupitia uwepo wa kituo hicho kwa kushirikiana na wananchi walifanikiwa kufikisha kero ya kukosekana kwa zahanati na eneo la kupimia watoto uzito ambapo walikuwa wakiwapima juu ya mti huku akina mama wajawazito wakipimwa katika ofisi ya mwenyekiti wa serikali za mtaa lakini baada ya kuiweka wazi kero hiyo hatimaye mbunge alifika eneo hilo na kuahidi kutoa milioni 50 ili kupatikana kwa zahanati katika eneo hilo na tayari ameanza kutimiza sehemu ya ahadi yake.

 Kwa upande wake mwenyekiti wa kituo cha taarifa na maarifa Majohe Tabu ALLY ameelezea changamoto ya viongozi wa serikali kuwachukulia wao kama watu ambao wanataka nafasi zao za uongozi kwani yeye alishakamatwa na kuwekwa rumande siku kadhaa na baadaye kuachiwa ambapo jambo hilo liliongeza ukaribu kati yake na viongozi baada ya kupata elimu juu ya kazi za vituo hivyo na kwa sasa wanashirikiana vyema na polisi katika kutokomeza vitendo vya ukatili Pamoja na kuchagiza maendeleo ya ujenzi ya matundu ya vyoo katika shule za kata hiyo na kufanikisha kuboreshwa kwa huduma za afya.

Kwa pamoja wenyeviti hao waliongeza kuwa vituo hivyo vimekuwa na mwamko mkubwa miongoni mwa wananchi na serikali kwa ujumla huku wakiyataja mafanikio kama vile kuongeza ushirikiano baina ya vituo na mamlaka za serikali katika utatuzi wa changamoto ikiwemo kutokomeza ukatili,ukeketaji na hata unyanyasaji huku wakiieleza changamoto za kimiundombinu ili kufika kwa wahanga wa vitendo vya ukatili pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya viongozi juu ya vituo hivyo

baadhi ya watangazaji na watayarishaji wa vipindi wakifuatilia warsha hiyo

 

 

 

 

 

 

Comments