Skip to main content

BRELA YAKUTANA NA TAASISI ZA UDHIBITI

  


NA MWANDISHI WETU

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), inakutana na Taasisi za Udhibiti ili kujadili mikakati ya pamoja ya namna ya kutatua mikinzano inayojitokeza katika utendaji kazi wa kila siku, kutokana na Sheria, Kanuni na Taratibu zinazozimamia Taasisi hizo hapa nchini.         

Akifungua Kikao Kazi  Kati ya BRELA na Taasisi za Udhibiti, leo tarehe 13 Septemba, 2023, katika ukumbi wa Nashera  Jijini Morogoro, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, ameeleza kuwa ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ni vyema kujadili kwa pamoja vikwazo vinavyosababishwa na usimamizi wa Sheria, Kanuni  na Taratibu zinazotumika na kuangalia jinsi ya kuvikwamua, ili kukuza uchumi wa Tanzania.     

 “Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuinua hali ya uchumi wa nchi, hivyo BRELA katika kuunga mkono jitihada hizo, inakutana nanyi ili kujadili mikinzano na muingiliano katika utoaji wa huduma na jinsi ya kuondokana na hali hiyo ili hatimaye kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa Tanzania hawakumbani na changamoto au uchelewaji wa kupata huduma  hapa nchini”, amesema Bw. Nyaisa.       

Ametoa mfano kuwa BRELA imekuwa ikikutana na changamoto katika utendaji na kusababisha usumbufu kwa wateja, pale ambapo Taasisi za Udhibiti zimekuwa zikitoa vibali vya biashara bila kujiridhisha endapo mfanyabiashara huyo amesajili Kampuni au Jina la Biashara ambapo athari kubwa anayoweza kuipata mfanyabiashara huyo endapo atapatiwa kibali wakati hajasajili Kampuni au Jina la Biashara ni kushindwa kusajili Jina la Biashara au Kampuni endapo jina husika litakuwa na ufanano na majina  yaliyokwisha sajiliwa BRELA, hivyo mhusika kulazimika kubadilisha jina husika.     

Ameendelea kusema kuwa athari kubwa anayoipata mfanyabiashara anaposhindwa kusajili jina linaloonekana kwenye Kibali alichokipata,  huathiri biashara yake kama vile kukosa zabuni, mikopo au kuingia mikataba na Taasisi za Umma, kwa kuwa usajili wa Jina la Biashara au Kampuni ni hitaji la msingi katika mfumo wa  sasa  wa Ununuzi unaosimamiwa na PPRA uitwao NEST,  ambao umeunganishwa na mfumo  wa usajili  kwa njia ya Mtandao( ORS) wa BRELA, ambapo  mfanyabiashara hataweza kujisajili katika mfumo wa NEST kama hajasajili Kampuni au Jina la Biashara.                         

 Naye, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw. Lazaro Msasalaga, amesema kuwa kikao kazi hicho ni muhimu maana kinatekeleza malengo ya  BluePrint  kwa kuzingatia umuhimu wa wafanyabiashara kuwa na Leseni ya Biashara inayotolewa na BRELA na leseni zingine zinazotolewa na Taasisi za Udhibiti ikizingatiwa kuwa sheria hizo zilikuwepo kabla ya andiko hilo.              

Washiriki wa Kikao Kazi  hicho kutoka Taasisi za Udhibiti ambao ni Wanasheria pamoja na Maafisa wanaohusika na utoaji wa vibali mbalimbali,  watapata fursa ya kujadiliana kwa siku tatu na kutoka na maazimio ambayo yatawasilishwa ngazi za juu ili  kufanyiwa kazi.    

BRELA, ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi tarehe 3 Desemba, 1999 ikiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Majukumu ya BRELA ni   pamoja na Kusajili majina ya Biashara, Kampuni, Alama za Biashara na  Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi “A”  na Utoaji wa Leseni za Viwanda na Vyeti vya Usajili wa Viwanda.

Comments