MAMLAKA ZA MAJI ZATAKIWA KUSHIRIKIANA VYEMA NA WADA KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA SEKTA HIYO

 



Mamlaka mbalimbali za maji nchini ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA] zimeshiriki mafunzo ya Bodi na Menejimenti za Mamlaka za maji yaliyofunguliwa na Waziri wa Maji, Mhe.Jumaa Aweso (Mb) yenye lengo la kujengea uwezo na ufanisi wa utendaji katika sekta ya maji Nchini.

Akizungumza katika mafunzo hayo Waziri Aweso amezitaka Mamlaka za maji kushirikiana na wadau mbalimbali Ili kupunguza changamoto na kuhakikisha sekta ya maji inasonga mbele.
"Hatuwezi kufanya kazi peke yetu, lazima tuhakikishe tunashirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea."ameeleza Mhe.Aweso.
Aweso ameongeza kuwa hivi sasa utekelezaji wa miradi unaendelea vizuri na jambo la kuzingatia ni utoaji wa huduma wa uhakika na taarifa kwa wateja zifike kwa wakati.
Sambamba na hayo DAWASA imeweza kuwa kati ya Mamlaka za maji zilizopanda daraja kutoka daraja A kwenda daraja AA na kutunukiwa cheti na Waziri Aweso.
Daraja AA hupewa kwa Mamlaka zenye vigezo ikiwemo upana wa mtandao wa zaidi ya asilimia 85 katika eneo la huduma, kumudu gharama za uendeshaji na matengenezo pamoja na uwezo wa kurejesha mtaji kwa mujibu wa Sheria Na.5 ya 2019 Kifungu Na.9 Cha Sheria ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira.
Mafunzo ya Bodi na Menejimenti za Mamlaka za Maji Tanzania Bara yanafanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Ubungo plaza kuanzia Septemba 25 hadi 26, 2023 na yamehudhuriwa na watendaji wakuu wa Wizara ya maji akiwemo Naibu Waziri wa Maji, Mhe Maryprisca Mahundi (Mb) na Katibu Mkuu wizara ya Maji, Profesa Jamal Katundu.

Comments