MADAKTARI WA SARATANI WATAKIWA KUONGEZA KASI YA UTAFITI KUPATA MBINU MPYA NA MBADALA ZA MATIBABU

 MADAKTARI WA SARATANI WATAKIWA KUONGEZA KASI YA UTAFITI KUPATA MBINU MPYA NA MBADALA ZA MATIBABU







NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, ametoa wito kwa taasisi, madaktari na masharika yanayotoa matibabu ya saratani kuongeza kasi ya kufanya tafiti za kisayansi zitakazosaidia kupata mbinu mpya na mbadala za matibabu.

Pia amesema makundi hayo yanatakiwa kuongeza kasi ya kutoa huduma zitakazowezesha wananchi kuhamasika kupata elimu ya namna ya kujikinga na kutambua mapema magonjwa ya saratani.

Prof. Paschal Ruggajo ambaye alimwakilisha, Waziri Ummy, alibainisha hayo leo jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa wa Saratani wa siku mbili ambalo linahusisha wataalamu wa matatibabu ya saratani duniani.

Ameongeza kuwa kutokana na takwimu za sasa kuonesha kwamba wanawake ndio wanaoathirika zaidi kwa maana kwa kila wanawake wanne wanaogundulika, mmoja huwa na saratani ya mlango wa kizazi ni sawa na asilimia 25.3 na wanawake 10 na mmoja anakuwa na saratani ya matiti na ni sawa na asilimia 9.9.

”Hivyo saratani hizo mbili hufanya kuwa sawa na theruthi moja sawa na asilimia 32.2 ya saratani zote zinazogundulika na zaidi umuhusu mwanamke na takwimu hizo ni kubwa na haikubaliki,” amesema.

Pia ameongeza kuwa takwimu zinaonesha uwepo wa wagonjwa wapya wa saratani wanaofikia 40,464 kila mwaka na vifo vinavyoripotiwa ni 27,000 hivyo ni dhahiri kuwa mikakati ya pamoja inahitajika ili kupunguza takwimu hizo.

Ameongeza kuwa wanaume nao hawajaachwa salama kwa maana saratani ya tezi dume huchangia kwa asilimia 8.8 na saratani zenye mlengo wa kijinsia inayofuata ni ya koo ambayo ipo kwa asilimia 6.5 na nyingine ni utumbo mpana ambayo ina asilimia 5.5 kwa wagonjwa wanaogundulika.

Amefafanua kuwa tafiti ambayo imefanywa na Tume ya Lancen nchini Marekani inaonesha kuwa athari za kiuchumi hapa nchini zinazotakana na saratani zinakadiriwa kuwa ni Sh. trilion 2.8 kwa mwaka.

”Takwimu ambazo zinatolewa ziwe chachu kutuhamasisha mtu mmoja mmoja, makundi na jamii kwa ujumla na kuanza kuchukua hatua ili kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama.

”Kupitia kongamano hili tunaamini mtajadiliana vema na mtawasilisha kwetu mapendekezo yenu ili kuishauri Serikali hatua za kuchukua katika kuboresha sera na miongozo ya matibabu ya saratani nchini.

“Nichukue nafasi hii kuwakumbusha watafiti na taasisi zetu zote ikiwemo NIMR, Vyuo vya Tiba, Hospitali na Taasisi nyingine kuhakikisha kuwa suala la kufanya utafiti na kuzitafsiri kuboresha huduma ni sehemu ya majukumu ya msingi ya Taasisi na Hospitali hizo, na wakati wote tafiti zilenge katika kutatua changamoto za jamii yetu na kuboresha miongozo na sera zetu za matibabu, amesema.

 Pia alisisitiza kwamba maamuzi ya njia sahihi ya matibabu kwa wagonjwa wa saratani yafanywe kwa pamoja kupitia Tumor Boards ambazo inapaswa ziimarishwe kwa maana ndio jukwaa sahihi la mjadala kuhusu chaguzi za matibabu, kufundishia wataalamu, kubaini maeneo ya tafiti na mapendekezo ya kuboresha miongozo ya matibabu ya saratani.

Ameongeza kuwa Tumor Board iboreshwe ili kuwa ya kimataifa na wataalamu saratani wa taasisi mbalimbali nchini waweze kufaidika na majadiliano hayo kwa kutumia maendeleo ya kiteknolojia na kimawasiliano vizuri na kuzingatia weledi na miiko ya kitaalumu katika kuhifadhi taarifa za mgonjwa.

Ameweka wazi kuwa Serikali ipo tayari kuendelea kuwekeza imeongeza kutoka sh. bilioni tano hadi nane kwa ajili ya upatikanaji wa elimu kwa madaktari namna ya kupambana na saratani.

Hivyo ametoa wito kwa daktari ambaye anahitaji kjiendeleza kielimu kutumia fursa hiyo kwa maana fedha za kutosha zipo kwa ajili hiyo ili kuboresha nyanja hiyo.

Naye, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Saratani Tanzania (TOS), Dkt Jerry Ndumbalo, amesema kongamano hilo linahusisha wataalamu wa saratani kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani ambao watabadilisha uzoefu na kuwasilisha machapisho ya tafiti ambazo zimefanywa.

”Machapisho ya tafiti hizo zimegusa maeneo mbalimbali ikiwemo uchunguzi, matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa baada ya kuanza matibabu jambo ambalo naamini litakuwa na tija,” amesema.

 Amefafanua katika kongamano hilo watajadili kwa pamoja namna ya kugundua saratani iliyo katika hatua ya awali na namna ya kuitibu kwa kutumia teknolojia mpya na namna ya kukinga.

 

Comments