Skip to main content

YUKO WAPI WARDA? WAZAZI WAMUOMBA RAIS SAMIA KUWASADIA KUPATIKANA KWA MTOTO WAO, DAU LA SHILINGI MILIONI 5 LATANGAZWA

 



Mama Mzazi wa Warda Muhamedi anayedaiwa kupotea Aprili 19 Mwaka huu Sakina Mtalika akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

 
Baba Mzazi wa Warda Muhamedi anayedaiwa kupotea Aprili 19 Mwaka huu Mohamedi Machamla akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi wa Taasisi ya Mapito Africa Foundation Zaliam Tabuyanjaa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Dada wa Warda Muhamedi anayedaiwa kupotea Aprili 19 Mwaka huu Sophia Mohamedi akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.

NA ABRAHAM NTAMBARA

WAZAZI wa Warda Mohamedi (16) ambaye anadaiwa kupotea tangu Aprili 19 Mwaka huu wamemuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kumpata mtoto wao akiwa hai au amekufa.

Pia Mkurugenzi wa Taasisi ya Mapito Africa Foundation, Zaliam Tabuyanjaa, ametangaza dau la Shilingi milioni 5 kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Binti huyo.

Inaelezwa kuwa Warda alipotea Kibaha mkoani Pwani akiwa anaishi kwa mlezi wake, anayetajwa kuwa ni mwalimu (jina limehifadhiwa) kwa zaidi ya miezi mitano.

Akizungumza na Waandishi wa habari Septemba 26, 2023 jijini Dar es Salaam Zaliam amesema kuwa awali walitangaza dau la shilingi milioni 3 kwa atakayefanikisha kupatikana kwa Warda ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Nyumbu iliyoko Kibaha mkoani Pwani bila mafanikio ya kupatikana kwake na sasa wameongeza kufikia shilingi milioni tano.

Wakati taasisi hiyo ambayo imezinduliwa rasmi jana jijini Dar es Salaam, ikitangaza dau hilo kupitia kwa Zaliam, ambaye ni mtangazai wa kipindi cha Mapito kinachorushwa na Global TV na Radio, Wazazi wa mwanafunzi huyo wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kuwasaidia kufanikisha kupatikana kwa mtoto huyo akiwa hai au amekufa.

“Namuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutusaidia kupatikana kwa mtoto wetu akiwa hai au amekufa, tunaamini kwa uwezo wake anaweza kuelekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya jitihada ya kufanikisha hili,” amesema Sakina Mtakila, mama mzazi wa binti huyo.

“Tangu tulipopata taarifa ya kupotea kwa binti yetu, April 19 mwaka huu akiwa kwa mwalimu wake aliyekuwa akimlea tangu akiwa darasa nne hadi sasa akiwa kidato cha pili, tulitoa taarifa Kituo cha Polisi Kibaha na kupewa RB Namba, KBA/ CID /PE/25/ 2023 – KOSA: JALADA LA UCHUNGUZI,”amesema.

Anasema baada ya kuripoti kituoni hapo mwalimu aliyekuwa akiishi naye alikamatwa na sasa yuko nje kwa dhamana na uchunguzi bado unaendelea ili kufanikisha kupatikana kwa binti huyo.

Inadaiwa sababu ya kupotea kwa mwanafunzi huyo ilitokana na Aprili 17 mwaka huu, kuonekana shuleni akiwa na simu ya mkononi, jambo ambalo ni kinyume na taratibu na sheria za shule na baada ya taarifa hiyo kumfikia mlezi wake (Mwalimu) aliadhibiwa kwa viboko hali iliyosababisha kutolala ndani na siku iliyofuata hakuonekana hadi leo.

Licha ya kuwepo madai ya kuonekana na simu mwanafunzi huyo akiwa shuleni , inaelezwa Mwalimu wa Nidhamu wa Shule hiyo, baada ya kuhojiwa na ndugu wa binti huyo waliokwenda shuleni hapo kupata ukweli alikanusha, Warda hakuonekana na simu kama inavyodaiwa na mlezi wake ambaye naye ni mwalimu.

Baba Mzazi wa mwanafunzi huyo, Mohamed Machamla, anasema alipata taarifa za kupotea binti yake April 22 mwaka huu, akiwa mkoani Mtwara anapoishi kwa sasa, na alipofanya mawasiliano kwa njia ya simu na mlezi wa mtoto wake (mwalimu), hakupewa ushirikiano wa kutosha kutokana na kukatiwa simu jambo lililompa mashaka na kuamua kufunga safari kwenda Kibaha mkoani Pwani kufuatilia suala hilo kwa kina.

Anasema licha ya kupata ushirikiano kwenye vyombo husika, bado nguvu inahitajika kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuongeza jitihada ya kufanikisha kupatikana kwa binti yake akiwa hali au mifupa kwani anapata maumivu makubwa akiona jambo hilo likiendelea kupigwa danadana na siku zikizidi kuyoyoma bila mafanikio na ametoa wito kwa majirani na wananchi wanaofahamu mazingira ya kupotea kwa binti yake wanapoitwa na vyombo vya ulinzi watoe ushirikiano bila hofu.

Awali, Zaliam amesema katika mchakato wa kumtafuta Warda wanatumia kauli mbiu inayosema YUKO WAPI WARDA? Na anawaomba wasamalia wema wenye taarifa sahihi za kupatikana kwa binti huyo kupiga simu namba 0689 498 684 au 0715 153 757.

Comments