WAZAZI WAASWA KUTORUHUSU MATUMIZI YALIYOPITILIZA YA SIMU KWA WATOTO, ILI KULINDA MAADILI.

 

Wazazi wametakiwa kuacha tabia ya kuwapa watoto wao uhuru uliopitiliza wa kutumia simu za mkononi, ambazo zinaweza kuwashawishi kufanya vitendo visivyo na maadili, kwa kuiga tabia hatarishi, zinazoweza kuharibu maisha yao ya baadae. 


Wakizungumza katika mahafali ya kuhitimu kidato cha nne kwa wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Bishop Thomas Labrecoue, baadhi ya wananchi wamesema kuwa wapo baadhi ya wazazi huwadekeza watoto na kuwaacha watumie simu bila kujali madhara yanayoweza kuwapata. 


“Kwenye simu kuna mambo mengi, yapo mazuri lakini pia yapo ambayo hayaendani na maadili na malezi ambayo wazazi tunahitaji kwa ajili ya watoto wetu, kwa hivyo vitu kama hivyo lazima wajiepushe navyo” amesema Jasson Mtayabagwe mkazi wa Muleba. 

Naye Anitha Fastine amesema kuwa wazazi wanayo matumaini makubwa kwa watoto wao na wanatamani baadae wawe watu wenye nafasi kubwa za kiuongozi na kiutawala, lakini kupitia kukua kwa teknolojia ikitumiwa vibaya inaweza kuwabadili na kuwapotosha, na kuwafanya wasitimize ndoto zao.


Kwa upande wake hakimu mfawidhi wa wilaya ya Muleba Daniel Pantaleo, amewataka wanafunzi hao kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na simu, maana huko kuna uchafu mwingi sana ambao wao kwa umri wao kuuepuka ni vigumu.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Saulo Malauli amewaasa wanafunzi kuendelea kuzingatia maadili waliyofundishwa shuleni, ili wawe mfano wa kuigwa katika jamii.


Sherehe hiyo ya kuhitimu kidato cha nne imeambatana na  ibada maalumu ya kuwaombea wanafunzi wa shule hiyo, ili wafanye vizuri katika mtihani wao wa taifa.

Comments