MAHAFALI YA 9 SHULE YA DALLAS KIDS ZONE; WAZAZI WATAKIWA KUTENGA MUDA KUWASIKILIZA WATOTO WAO

wahitimu wa darasa la awali katika shule ya awali ya Dallas kidszone day care,nursery school wakiwa kwenye picha ya pamoja 









Na PrayGod Thadei,Dar es salaam

 Wazazi na walezi hapa nchini wametakiwa kutenga sehemu ya muda wao na kuwa na utaratibu wa kukaa muda wa kutosha na kuzungumza na watoto wao ili kufahamu changamoto wanazopitia.


Hayo yamesemwa na mdhibiti mkuu wa ubora wa shule wilaya ya Temeke Lilian Kazenga alipokuwa akizungumza katika sherehe za mahafali ya 9 ya shule ya awali ya Dallas Kids Zone daycare &nursery yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC)jijini Dar es salaam ambapo amesema wazazi na walezi wengi wa siku hizi wamekuwa hawatengi muda wa kukaa na watoto wao na badala yake jukumu hilo wameliacha Kwa shule pekee.

Alisema kutokana na wazazi kutotoa muda wa kutosha kukaa na kuzungumza na watoto wao hali hiyo imepelekea watoto wengi kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo ulawiti na ubakaji na wakakaa kimya na kukosa wa kuwaambia changamoto wanazopitia.

"tutoe muda wa kuwasikiliza watoto kwani mashuleni siyo salama,mtaani siyo salama na hata majumbani siyo salama kwani ndugu tunaodhani ni watu wazuri wamekuwa maadui wa kwanza kwa watoto wetu majumbani hivyo niwasihi wazazi tuwe tunawasikiliza watoto wetu dunia ya sasa siyo salama"alisema 




Aidha Bi Kazenga aliwapongeza wazazi kwa kuichagua shule ya awali ya Dalas kama sehemu ya watoto wao kupata elimu ya awali kwani ni shule iliyozingatia taratibu zote za utoaji elimu ikiwemo kuwafundisha watoto maadili mema na dini jambo ambalo limewajengea watoto hao ujasiri.

Kwa upande wake Dkt Rehema Chande Mallya ambaye ni mkurugenzi wa shule za Dallas kids zone daycare & nursery alisema shule hiyo yenye kampasi zake Mlimani city na Kigamboni imekuwa ikiwajengea watoto uwezo mkubwa kiakili na kitaaluma na wamefanya mafunzo ya maadili mema kama nguzo ya kuwajenga watoto.
Alisema wanafunzi wa darasa la awali wa shule hiyo wamekuwa wakifanya vizuri kimasomo hata waliposhindanishwa na wanafunzi wa shule nyingine jambo lililochagizwa na ubora wa elimu itolewayo

Hata hivyo Dkt Rehema aliwashukuru wazazi na walezi kwa kuichagua shule hiyo kwa kuwapeleka watoto wao huku akiahidi kuendelea kutoa elimu bora itakayopelekea wazazi hao kuwa mashahidi kwa wazazi wengine kwa elimu bora inayotolewa shuleni hapo huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu kwa shule za umma na binafsi hapa nchini

Comments