PROF. TIBAIJUKA ATAKA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA UONGOZI
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umefanya Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati Dhidi ya Ukatili wa Kijinsia yakiongozwa na kauli mbiu ya “Wekeza Rasilimali, Kutokomeza Ukatili na Kuongeza Ushiriki wa Wanawake kwenye Nafasi za Uongozi” kwa lengo la kutambua, kusherehekea na kushirikishana uzoefu na mbinu mbalimbali za kuimarisha harakati za kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini Tanzania.
Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wenyeviti wa Halmashauri na Madiwani,Viongozi kutoka Vyama vya Siasa, Taasisi za Umma asasi za kiraia ,Viongozi wa Dini,watia nia na wanawake viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo yamefanyika leo Jumatano Desemba 6,2023 katika Ofisi za TGNP, Mabibo Jijini Dar es salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Prof. Anna Tibaijuka.
Katika maadhimisho hayo, washiriki wamefanya mijadala yenye manufaa na tija katika kuweka mikakati ya kuwekeza ikiwemo, kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, utakaoacha alama kwa vizazi vijavyo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Prof. Anna Tibaijuka amesema dhana ya ushiriki wa wanawake katika uongozi na ngazi za maamuzi na utengwaji wa rasilimali ni chachu ya kuleta usawa na kutokomeza ukatili wa kijinsia hivyo wanawake wakishiriki katika meza za maamuzi upo uwezekano mkubwa wa masuala ya usawa wa kijinsia kupewa kipaumbele, kutokana na kuwa masuala hayo yanawaathiri moja kwa moja.
Prof. Tibaijuka amesema endapo wanawake watakuwa wengi Bungeni kuna uwezekano mkubwa wa sheria na sera zinazotungwa na kupitishwa bungeni zikawa na mitizamo ya kijinsia na zile zinazowakandamiza wanawake na makundi mengine zikarekebishwa kwa haraka zaidi.
Prof. Anna Tibaijuka akionesha Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Prof. Tibaijuka ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuweza kukabiliana na ukatili dhidi ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum huku akitoa rai kwa jamii kutofumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani vitendo hivyo vinaumiza, vinadhalilisha, vinapunguza uzalishaji na vinaathiri uchumi kwa kuongeza gharama kwa familia, jamii na Serikali.
Katika hatua nyingine ameipongeza TGNP kwa kuwa kinara katika jitihada za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum na kuwaandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Katika maandalizi ya kuelekea uchaguzi 2024/25, TGNP imezindua Ilani ya Wanawake yenye lengo la kutoa madai ya wanawake kwa watia nia na wagombea wakati wa uchaguzi 2024/25, hatua hii ni ya muhimu sana. Ni matumaini yangu kuwa kitabu hiki kitatumika vizuri katika kuhakikisha kuwa ajenda za wagombea 2024/25 zinabeba madai yaliyobainishwa katika Ilani hii. Hongera sana TGNP”,amesema Prof. Tibaijuka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Bi. Gemma Akilimali amesema Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu ya kitaifa isemayo “Wekeza: Kupinga Ukatili wa Kijinsia” Na wakati huo huo TGNP ikiwa na mada isemayo “Wekeza Rasilimali, Kutokomeza Ukatili na Kuongeza Ushiriki wa Wanawake kwenye Nafasi za Uongozi” ambayo ni mada mahususi kwani kwa sasa nchi ya Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2024/2025.
“Jukwaa hili la leo limejikita katika kujadili, kutathmini na kuandaa mikakati yenye lengo la kuwekeza rasilimali na ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi. Vilevile, Jukwaa hili linatupa fursa ya kujadili kwa kina mikakati iliyowekwa, pamoja na kuendelea kuhamasisha utengwaji wa bajeti yenye mrengo wa kijinsia katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia, kuongeza wanawake katika nafasi za uongozi, hususani kwenye michakato ya uchaguzi inayotarajiwa kuanza mwaka 2024”,amesema Bi. Akilimali.
“Usawa wa kijinsia ni msingi katika kujenga dunia tuipendayo; na dunia tuipendayo ni dunia isiyo na ukatili kwa wanawake, Watoto na makundi maalum. Hilo linawezekana tu ikiwa kila mmoja wetu katika nafasi yake, atachukua hatua sasa, kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia”,ameongeza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Bi. Lilian Liundi amesema upo uhusiano mkubwa kati ya uwekezaji wa rasilimali kwa mrengo wa jinsia na uwezo wa kukabiliana na masuala ya ukatili wa kijinsia.
“Tunapozungumzia uwekezaji hatuna maana ya rasilimali fedha tu, bali ni kuanzia kwenye uwekezaji wa mazingira wezeshi ya kisera, kisheria, mipango na bajeti kwa mrengo wa kijinsia. Tukianzia hapo tutatengeneza Sera, sheria, mipango, bajeti inayoaangalia mahitaji ya makundi yote katika jamii na tutaweza kutatua changamoto bila kumwacha mtu, kwa kiwango kikubwa”,amesema Liundi.
Amebainisha kuwa ,Uwekezaji unaanzia katika ngazi ya mtu binafsi, familia, jamii na hata taifa kwa ujumla na kwamba uwekezaji wa kupata taarifa sahihi kwa wakati, uwekezaji wa muda, uwekezaji wa ujuzi na maarifa, uwekezaji wa vifaa vya kuwezesha kutatua changamoto ni muhimu sana pia.
Amesisitiza kuwa, Uwekezaji wa rasilimali katika kuandaa viongozi kwa jicho la kijinsia wakiwemo wanawake, wanaume na makundi maalum nalo ni suala linalohitaji mkakati na dhamira ya dhati.
“Ili kutengeneza viongozi bora bila kubagua tunahitaji uchambuzi wa kina wa mahitaji ya makundi yote na uwekezaji wa kutosha ili kuwa na viongozi bora watakaoendesha siasa safi na kuwasaidia wananchi (watu). Katika zama hizi tuna changamoto kubwa sana ya kuwa na viongozi ambao sio watumishi wa watu ila wanajitumikia wao na matumbo yao na watu wachache waliokaribu yao. Ndio maana tuna tatizo kubwa la rushwa, kutokuwa na uwajibikaji, matumizi mabaya ya madaraka, hii inasababisha watu wengi kuachwa nyuma katika maendeleo”,ameongeza Liundi.
Katika hatua nyingine amesema TGNP kwa kushirikiana na wadau wake imekuwa ikifanya afua mbalimbali zenye lengo la kuwaandaa wanawake kuwa viongozi bora na kwa upande mwingine kuelimisha jamiii juu ya umuhimu wa wanawake na makundi maalum katika jamii, ili kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo kubadilisha mitizamo kandamizi na mila potofu dhidi ya wanawake kuwa viongozi, pamoja na kuwapunguzia wanawake mzigo mkubwa wa majukumu ambao unasabisha umaskini wa muda na kipato.
"Ni muhimu sana kuwekeza rasilimali katika kutatua changamoto za kijinsia ikiwemo ukatili wa kijinsia. Ikumbukwe kuwa suala la usawa wa jinsia ni suala la maendeleo na si vinginevyo. Dunia inapoteza mapato mengi kwa kutokuzingatia usawa wa kijinsia. Ni ukweli usiopingika kuwa ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi na uongozi kwa njia moja au nyingine ni chachu ya kutokomeza au kupunguza ukatili wa kijinsia",amesema.
Aidha amesema upo umuhimu kuendelea kuelemisha jamii kuwa na matumizi sahihi ya mitandao badala ya kuchafua wagombea, kutumia mitandao kunadi sera zao na kuonyesha mazuri waliyofanya ili kuweza kushawishi umma kuwachagua.
"Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia nayo hayajatuacha salama, yamekuja na aina mpya za ukatili wa jinsia hususani wa kwenye mitandao. Tunapoelekea kwenye uchaguzi wa 2024/25, ni muhimu kuchukua hatua za haraka kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii inayokua kwa kasi sana. Ikumbukwe kuwa kwa kiwango kikubwa teknolojia ya habari na mawasiliano itatumika sana kwa kipindi hicho na kama hatutachukua hatua za haraka kuthibiti ukatili wa kimtandao, wanawake watia nia na wagombea watakatiliwa sana kupitia mitandao",ameeleza Liundi.
Aidha Liundi ameipongeza Serikali kwa juhudi za kuendelea kutekeleza mikakati ya kutokomeza ukatili wa jinsia huku akitoa wito kwa Serikali, wadau wa maendeleo na Asasi za Kiraia,kuwekeza rasilimali za kutosha katika kuhakikisha utekelezaji wa MTAKUWWA II, ili kuweza kukabiliana na janga hili la ukatili wa kijinsia.
"Usawa wa kijinsia ni suala la maendeleo na ukatili wa kijinsia ni moja ya kikwazo kikubwa kufikia usawa huo. Kwa pamoja,hatuna budi, kutoa kipaumbele ili kuongeza ushiriki wa wanawake wenye tija katika Maendeleo", amesema Liundi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Mkoani Morogoro, Rachel Nyangasi amesema bado kuna baadhi ya wazazi wanawataka watoto wao wafeli kwenye mitihani ili wakafanye kazi za ndani na watoto wengine kuachiwa majukumu ya kulea familia kama watu wazima hivyo ipo haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo katika Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Diana Masesa ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyoliwekea mkazo suala la usawa wa kijinsia huku akisisitiza umuhimu wa wanaume kushirikishwa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Nao washiriki wa maadhimisho hayo wameshauri wanawake kuwania nafasi za uongozi na kushiriki katika ngazi za maamuzi na kwamba kwa wale wanaotaka kushika nafasi za uongozi katika vyama vya siasa ni vyema wakawa na utamaduni wa kushiriki katika shughuli za vyama badala ya kusubiri kuingia kwenye
"Msiogope kufyeka misitu, msisubiri kuingia kwenye siasa wakati wa mchakato wa uchaguzi tu....Majimbo yanatengenezwa",amesema Katibu Ngome ya Wanawake ACT Wazalendo Bonifasia Mapunda.
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) leo Jumatano Desemba 6,2023 katika Ofisi za TGNP Mabibo Jijini Dar es salaam. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka akionesha Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka na viongozi meza kuu wakionesha Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mgeni rasmi Prof. Anna Tibaijuka akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Bi. Gemma Akilimali (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Bi. Lilian Liundi (kulia).
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Bi. Gemma Akilimali akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Bi. Gemma Akilimali akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Bi. Lilian Liundi akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Afisa Maendeleo katika Ubalozi wa Canada nchini Tanzania, Diana Masesa akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP
Comments