Skip to main content

JUHUDI ZA MHESHIMIWA RAIS ZIMETUONGEZEA KASI YA KUKUZA UTALII NGORONGORO- KAMISHNA KIIZA

 

JUHUDI ZA MHESHIMIWA RAIS ZIMETUONGEZEA KASI YA KUKUZA UTALII NGORONGORO- KAMISHNA KIIZA



Na Mwandishi wa NCAA, Karatu Arusha.

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Bw.Richard Kiiza amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan imeongeza kasi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.

Akizungumza na waandishi wa habari wa kituo cha utangazaji cha Clouds Media waliofika Ngorongoro kufanya tathmini ya juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kutangaza utalii, Bw.Kiiza amesema watalii wamekuwa wakitembelea Ngorongoro kwa idadi kubwa na hivyo kuongeza wigo wa mamlaka hiyo kufanya kazi usiku na mchana ili kusimamia juhudi zilizofanywa za kuutangaza utalii.

Takwimu kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro zinaonesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba, 2023 jumla ya watalii 534,065 wametembelea hifadhi hiyo ambapo wageni kutoka nje ni 335,340 na wageni kutoka ndani ya nchi ni 198,725. Aidha katika kipindi hicho cha nusu mwaka zaidi ya shilingi bilioni 123 zilikusanywa na kuingia kwenye mfuko mkuu wa Serikali.

Kamishna Kiiza ametoa wito kwa watanzania kuendelea kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro ili kujionea vivutio mbalimbali ambavyo vipo ndani ya hifadhi na hivyo kutoa fursa kwa wananchi kujifunza kuhusu uhifadhi wa rasilimali za nchi.
 
Kamishna huyo wa Uhifadhi ameongeza kuwa Uongozi wa NCAA utaendelea kuboresha miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi ili kuhakikisha kuwa wageni wote wanaotembelea hifadhi hiyo wanapata huduma nzuri kwa wakati.

Mkuu wa msafara kutoka Clouds media Bw.Pancras Mayala alisema kuwa kituo hicho cha utangazaji kimeamua kutembelea maeneo mbalimbali ya hifadhi ili kujionea jinsi serikali ya awamu ya sita kupitia filamu ya _Tanzania the Royal Tour_ ilivyosaidia kukuza utalii hapa nchini.

Comments