MSOMERA:KIJIJI KILICHOBADILISHA MAISHA YA WALIOHAMA KUTOKA NGORONGORO

 


Wananchi wakiwa mbele ya kibao Cha Ofisi ya posta lililopo katika Kijiji Cha Msomera wilayani Handeni walipohamia wananchi kutoka wilayani Ngorongoro

Jengo la ofisi ya posta lililopo katika Kijiji Cha Msomera wilayani Handeni walipohamia wananchi kutoka wilayani ya Ngorongoro.



Na PrayGod Thadei,Ngorongoro,Msomera


Ni wazi sasa maisha ya waliokuwa wakazi wa hifadhi ya Ngorongoro ambao walikubali kuhama kwa hiari na kuhamia katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni,Mkoani Tanga yameimarika mara baada ya wakazi hao ambao wengi wao ni kutoka jamii ya Kimasai ambao hapo awali walikuwa ni wafugaji pekee wasio na mashamba ya kulima kuanza kujihusisha na kilimo.

Kupitia ziara ya waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari zaidi ya 58 hapa nchini waliotembelea Katika hifadhi ya Ngorongoro na baadaye kijiji cha Msomera na kujionea mashamba makubwa ya mahindi katika kijiji hicho hilo ni dhihirisho tosha kuwa wakazi hao sasa wameanza maisha mapya. 

Katika ziara hiyo ya siku nne,waandishi hao wakiwa wameambatana na baadhi ya Maafisa kutoka mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ndani ya hifadhi hiyo walishuhudia binadamu na wanyama wakiishi eneo moja,jambo ambalo ni hatari kwao.

Ndani ya hifadhi hiyo kulishuhudiwa kundi la wanyama pori aina ya Pundamilia likiwa katikati ya na kundi la ng'ombe huku watoto wadogo wakionekana kuchunga mifugo hiyo.

Hata hivyo siyo tu kundi la ng'ombe lililochanganyika na kundi la wanyamapori 'pundamilia'lililowashangaza waandishi wa Habari hao bali walishuhudia pia kundi la wanyama hao likiwa katikati ya shule moja ya sekondari,huku wanafunzi wakiendelea na masomo.

Ziara ya waandishi hao ambao walitembelea vijiji 11 katika kata 4 za Tarafa ya Ngorongoro na kushuhudia maisha duni wanaoishi wakazi hao ambao kwa mujibu wa sheria ya hifadhi za Taifa hawaruhusiwi kufanya shughuli yoyote ndani ya hifadhi ikiwemo kilimo jambo lililoipelekea serikali kuwapa fidia na kuwatafutia maeneo mengine ya kuishi,kuwajengea nyumba,kuwapa mashamba ya kilimo na malisho pamoja na shilingi milioni 10 hadi 15 kwa ajili ya kuanza maisha mapya.

Safari ya waandishi hao wa Habari ambayo ilianzia jijini Dar es salaam,iliondoka wilayani Ngorongoro kuelekea wilayani Handeni, kijijini Msomera ili kujionea hali halisi ya baadhi ya wananchi waliohamia kwa hiari katika kijiji hicho kutokea Ngorongoro ambapo walishuhudia nyumba za kisasa zilizojengwa na ambazo zinaendelea kujengwa pamoja na mashamba yaliyosheheni mazao ya mahindi huku wakaazi wa kijiji hicho wakiendelea na shughuli zao ikiwemo biashara.

Bwana Saiboko Laizer ambao ni mmoja wa wananchi waliohamia kwa hiari kutoka Ngorongoro na kwenda kuanza maisha mapya katika kijiji hicho ambaye kwa sasa anajihusisha na kilimo,ufugaji pamoja na kumiliki mashine ya kusaga na kukoboa nafaka aliwaambia waandishi wa Habari kuwa kwa  sasa anaishi kwa amani bila wasiwasi wowote kwani wanatembea muda wote na kujihusisha na shughuli za kimaendeleo ambazo walikuwa hawawezi kuzifanya wakiwa Ngorongoro kutokana na sheria za hifadhi hiyo ambazo humruhusu mtu kutembea kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni pekee jambo ambalo liliwafanya kuishi maisha duni na ya hofu.

"kama mnavyoona hapa mimi nilikuwa nakaa tu nyumbani bila kufanya kazi nikiwa kule Ngorongoro lakini hapa Msomera sasa ninaendesha maisha yangu vizuri na ninamiliki mashine ya kukoboa na kusaga nafaka"alisema

Laizer aliendelea kusema kuwa kijiji cha Msomera kimekuwa ni kijiji cha mfano kwa maendeleo hapa nchini kwani tayari serikali imewapelekea huduma za afya,shule za kisasa,umeme,maji na kuwajengea barabara.

Hata hivyo Laizer ameiomba serikali kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wakazi waliobaki Ngorongoro juu ya hatari ya kuishi hifadhini na faida na fursa zilizopo Msomera ili iwe rahisi kwa wao kuhama ndani ya hifadhi hiyo.

Si Laizer pekee anayefurahia maisha kijijini Msomera,Bi Aveline Kimrei ambaye anafanya kazi katika ofisi ya Posta ya kijiji hicho alisema kuwa Kijiji hicho kimebadili maisha yake kwani sasa anafanya kazi katika ofisi ya Posta ambapo hapo awali akiwa Ngorongoro hakuwa akijishughulisha na shughuli yoyote ya kiuchumi.

Alisema kuwa wananchi wa Kijiji hicho wamehamasika kwa kiasi kikubwa kutumia huduma za posta kwani zipo karibu na wao na wanazipata kwa wakati tofauti na Ngorongoro ambapo walilazimika kwenda umbali mrefu ili kupata huduma hiyo.

 

 Bi Sara Yohana ambaye ni mmoja wa wananchi wa Kijiji hicho alisema kuwa kwa sasa wanalima mazao ya mahindi na pia wanatarajia kuvuna mazao ya kutosha kwa ajili ya chakula kwani hawakuwa na mashamba wala kuweza kulima wakiwa Ngorongoro.

Bi Sara aliishukuru Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na serikali kwa kuwapa eneo ambalo lina ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo na kuwapelekea huduma zote muhimu ikiwemo za afya,elimu,posta na miundombinu ya barabara na maji.

"maisha ya hapa siyo mabaya kwani hapa kuna fursa ya kilimo na biashara na tuna uhuru wa kutembea muda wowote tunaotaka,usiku na mchana na tumejengewa nyumba za kisasa"alisema.

Awali akizungumza na waandishi wa Habari hao,Msemaji mkuu wa serikali alisema mpaka sasa kaya zaidi ya 126 zenye watu zaidi ya 812 tayari zimehamia katika jijiji hicho huku kaya nyingine 72 zikiwasili jana katika kijiji hicho ambacho kutajengwa nyumba 2559.

Alisema Shukrani za juhudi zote zinazofanyika katika eneo hili la Msomera, zinaelekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiyo aliyeidhinisha pori hili la akiba kujengwa makazi mapya," amesema Matinyi.

Matinyi alisema kuwa Katika eneo hilo, zimepangwa zijengwe barabara zenye urefu wa KM 800 ambapo mpaka sasa KM 150 zimekamilika huku mpaka sasa jumla ya visima 10 vikiwa vimeshachimbwa na vingine vinaendelea kuchimbwa na umeme umeanza kusambazwa.

Kwamba Shule ya Msingi imeshakamilika huku Shule ya Sekondari ya kisasa yenye maabara za masomo ya sayansi, TEHAMA na maktaba, Zahanati, Kituo cha Polisi vikiendelea kujengwa. 
 
Amebainisha kuwa katika eneo hilo Mnada umeshajengwa, malisho ya mifugo yameshapimwa na vituo vya kuuzia maziwa vinaendelea kujengwa.

Sambamba na hilo amesema Mawasiliano tayari yameshafikishwa na hatua inayofuata ni Mfuko wa Mawasiliano Tanzania kuendelea na usambazaji wa minara ya mawasiliano kwa kushirikiana na kampuni binafsi za simu. Vile vile amebeinisha kuwa Majosho yanaendelea kujengwa huku upimaji wa viwanja unaendelea.

Amesema katika awamu ya pili, kufikia Januari 12, 2024, kaya zilizojiandikisha kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro ni 525, kati ya kaya hizo, 126 zenye watu 812 na mifugo 2,581 tayari zimeshahama. 

Kwamba Kaya zilizohama zimegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza lenye kaya 74 lenye watu 520 na mifugo 1,599 limekuja Msomera na kundi la pili la kaya 52 lenye watu 292 na mifugo 982 wamechagua kwenda kwenye mikoa mbalimbali.

"Kwa ujumla wake, mpaka sasa kaya 677 zimeshahama kwa hiari kutoka Ngorongoro zikiwa na watu 3,822 na mifugo 18,102. Zoezi la uhamaji kwa hiari linaendelea, Januari 18, 2024, kutakuwa na kundi lingine la kaya 72 lenye watu 515 ambalo litaondoka Ngorongoro. Ujenzi wa nyumba 1,000 uko katika hatua mbalimbali za ukamilikaji wake," ameeleza Matinyi.

Matinyi amesema uondokaji wa wananchi kutoka Ngorongoro kwenda Msomera kutasaidia eneo la Ngorongoro kuondoa tatizo la mmomonyoko wa ardhi na uchafuzi wa aina ya mimea pamoja na kuondoa tatizo la magonjwa ya wanyamapori kuingiliana na mifugo.

"Nawashauri wote wenye mashaka na zoezi la kuhamisha watu kutoka Ngorongoro waje wauone ukweli na baada ya hapo wenye nia njema watasema ukweli. Serikali ina nia njema, hakuna muda ambao itakaa chini kwa ajili ya kufanya maamuzi yatakayoumiza wananchi wake," ameeleza Matinyi.



Comments