ACT WAZALENDO YAELEZA MWITIKIO MDOGO WA WANAWAKE KUWANIA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA HICHO.
Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam.
Licha ya Wanawake kupewa kipaumbele kuwania nafasi mbalimbali za uongozi bado kuna uzito kwa Wanawake kujitokeza kushiriki kwenye vikao vya maamuzi hata vinavyohusisha Wanawake wenyewe .
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Joran Bashange wakati akitoa taarifa ya zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama.
Amesema chama hicho kimepitisha sera ya jinsia na kuchukua hatua mahususi katika chaguzi zake Kikatiba na kikanuni ambapo kumekuwa na mchango mkubwa katika kusaidia Wanawake kuingia kwenye vikao vya maamuzi.
"Mfano hai tunaonana kwenye uchukuaji fomu za kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama zilizohitimishwa Jana ambapo kwenye uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi 6 za uongozi wa juu wa Chama Ngome ya Wanawake ni Wanawake 15 tu wamejitokeza ikilinganishwa na ngome ya Wazee waliojitokeza ni 30 hii inadhihirisha kuwa mwamko bado ni mdogo Kwa Wanawake” Amesema Bashange.
Ameongeza kuwa jumla ya nafasi 70 zinazowaniwa ndani ya chama hicho tayari wagombea 179 wamerejesha fomu huku nyingine wakiendelea kuzipokea.
Hata hivyo amesema kabla ya kufanyika Kwa uchaguzi Mkuu wa Chama hicho watafanya midahalo mbalimbali Kwa watia nia kutoa sera zao ambapo mdahalo wa Ngome ya Vijana unatarajiwa kufanyika tarehe 27 mwezi huu na baadae Ngome ya Wanawake 28 na kifuatiwa na mdahalo wa watia nia katika nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Chama Mwenyekiti na Makamu wenyeviti utakaofanyika Machi 4/2024 ambapo midahalo yote itafanyoka katika ofisi za makao makuu ya Chama Dar es Salaam.
Comments