Skip to main content

KITITA CHA MAFAO KWA WANUFAIKA NHIF KUANZA RASMI MACHI MOSI

 KITITA CHA MAFAO KWA WANUFAIKA  NHIF KUANZA RASMI MACHI MOSI 




Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Berna Konga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


NA PRAYGOD THADEI


Katika kuhakikisha na kufanikisha watanzania kuendelea kupata huduma za afya kupitia bima,MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umefanya maboresho ya Kitita cha Mafao kwa wanachama wake ambayo utekelezaji wake utaanza rasmi Machi 1, 2024.

Akitoa taarifa ya kuanza kutumika kwa kitita hicho cha mafao kwa wanachama wake,leo Februari 28, 2024  katika mkutano na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Berna Konga amesema kitita hicho cha mafao ni orodha ya huduma za matibabu zinazotolewa kwa wanaufaika wa mfuko wa NHIF.

“Kitita cha mafao ni orodha ya huduma za matibabu ambazo zinatolewa kwa wanufaika wa NHIF na bei zake ambazo hutumika wakati wa malipo kwa madai ya watoa huduma za matibabu. Maboresho ya mwisho ya kitita cha mafao cha NHIF kinachotumika sasa yalifanyika Juni, 2016 takriban miaka nane iliyopita na hivyo kuwepo kwa umuhimu wa kufanya marejeo yake kutokana na sababu mbalimbali kama zinavyoanishwa kwenye taarifa hii,” amesema Konga.

Kuhusu malengo ya kitita hicho Bw Konga ametaja kuwa ni kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama ikiwa ni pamoja na kuongeza huduma ambazo hazikuwepo awali, Kufanya maboresho ya huduma na gharama zake kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia na hali halisi ya bei katika soko na Kuwianisha Kitita cha Mafao na miongozo ya tiba iliyoboreshwa ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanufaika wa Mfuko.


Malengo mengine ni Kujumuisha maoni na mapendekezo mbalimbali ya Wadau, Kutekeleza ushauri wa Taarifa ya Mapendekezo ya Tathmini ya Uhai na Uendelevu wa Mfuko kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2021 na  Kuimarisha udhibiti katika mianya ya udanganyifu.


Konga ameeleza kuwa Mfuko ulianza zoezi la kufanya marejeo ya kitita kuanzia mwaka 2018, hata tenhivyo utekelezaji wa kitita kipya haukufanyika kutokana na uhitaji wa kuhusisha wadau zaidi ili kuwa na uelewa na maoni zaidi kuboresha kitita hicho. 


Maboresho ya Kitita cha Mafao yamehusisha kufanyika kwa Tathmini ya Uhai na Uendelevu wa Mfuko na kutekeleza mapendekezo yake ambapo tathmini ya mwisho ilifanyika Juni, 2021 ambapo Kifungu Na 15.2 cha Mkataba baina ya Mfuko na Watoa Huduma kinautaka Mfuko kutoa notisi ya miezi mitatu (3) ya kusudio la kufanya maboresho katika kitita chake kabla ya kuanza kutumika.

Amesema katika kutekeleza takwa hilo la mkataba, 1 Agosti 1, 2022 Mfuko kupitia barua yenye Kumb. Na. EA.35/269/01-A/32 ulitoa Notisi ya miezi mitatu (3) ya kusudio la kufanya maboresho ya Kitita chake cha Mafao ambapo tangu tarehe ya kutolewa kwa Notisi hiyo, Mfuko uliendelea kushirikisha wadau, kukusanya na kupokea maoni, ushauri na mapendekezo kutoka kwa wadau wake kwa lengo la kuboresha Kitita chake cha Mafao ambapo kwa nyakati tofauti Mfuko ulifanikiwa kukutana na Watoa Huduma za Matibabu wa Umma na Binafsi na Madhahebu ya Dini na Vyama mbalimbali vya taaluma za afya.

Konga ametaja maeneo yaliyofanyiwa mapitio na maboresho katika Kitita cha Mafao ni pamoja na ada ya usajili na kupata ushauri wa daktari, huduma za dawa, huduma za vipimo, huduma za upasuaji, na gharama za kliniki za kawaida na kibingwa.

Comments