LAIGWANAN EDWARD LOWASSA AZIKWA KIJIJINI KWAO.

 




Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Ngoyai Lowassa, umezikwa leo Jumamosi katika kijiji alikozaliwa kaskazini mwa taifa hilo wiki moja baada ya kuaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ndiye aliwaongoza maelfu ya waombolezaji kwenye mazishi hayo ya Lowassa yaliyofanyika katika kijiji cha Ngarash kilichopo wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Katika hotuba yake mbele ya waombolezaji kabla ya mazishi, Rais Samia amemuelezea hayati Edward Lowassa, kuwa mwanasiasa aliyetumia nusu ya maisha yake kulitumikia taifa  hilo la Afrika Mashariki, na ameacha alama kubwa kutokana na utumishi wake aliosema "umetukuka."

Rais Samia pia ameeleza kwamba Lowassa alikuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za nchi , hali iliyomuwezesha kupata kura nyingi za urais kuliko mgombea mwingine yeyote wa chama cha upinzani tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini Tanzania. 

Lowassa, kada wa siku nyingi wa chama tawala nchini Tanzania, CCM, alikihama chama hicho mwaka 2015 na kugombea kiti cha urais kupitia upinzani. Alipata asilimia 40 ya kura katika uchaguzi ambao John Magufuli, aliyewania kupitia CCM alishinda kiti cha urais kwa asilimia 58 ya kura na baadaye 2019 alirejea tena ndani ya CCM 

Comments