MARUFUKU YA VING'ORA NA VIMULIMULI KWENYE MAGARI BINAFSI YATANGAZWA,WATAKAOKAMATWA KUKIONA

 MARUFUKU YA VING'ORA NA VIMULIMULI KWENYE MAGARI BINAFSI YATANGAZWA,WATAKAOKAMATWA KUKIONA






Na Mwandishi wetu,

Jeshi la Polisi nchini Kupitia  kikosi cha Usalama Barabarani limepiga marufuku matumizi ya ving'ora na vimulimuli kwa wamiliki na madereva wote wa magari binafsi nchini 

Marufuku hiyo imetolewa leo IjumaaFebruary 23,2023 ambapo jeshi Hilo limewataka watanzania Kutoweka Ving'ora, Vimulimuli, Namba bandia na taa za kuongezwa kwenye magari na pikipiki na Kama kuna ulazima wa kufanya hivyo basi wanatakiwa kuomba ridhaa ya kupata kibali cha kufanya hivyo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Kupitia marufuku hiyo jeshi Hilo limesisitiza kuwa litaanza oparesheni kabambe ya kukamata magari yote na pikipiki ambayo si ya dharura na yamefungwa ving'ora bila kuzingatia utaratibu wa kisheria kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukulia dhidi yao ikiwemo kupelekwa mahakamani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, DCP Ramadhani Ng'anzi amesema kuwa ni kinyume cha sheria kwa mtu yoyote kufunga king'ora katika gari au pikipiki bila kuzingatia utaratibu wa kisheria na kanuni za usalama barabarani zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

"Wapo baadhi ya wananchi ambao wamegeuza ving'ora kuwa fasheni  katika magari au pikipiki zao, tukumbuke kuweka king'ora cha aina yoyote katika gari au pikipiki ni lazima ufuate sheria tutawakamata kuanzia leo wote watakaokaidi agizo hili na tutawachukulia hatua"amesema Kamanda Ng'anzi.

Aidha, amesema kuwa,kuna baadhi ya watu, makampuni na taasisi mbalimbali zimekuwa zikivunja sheria ya usalama barabarani, na  wanastahi adhabu ikiwemo ya kulipa faini ya tozo za makosa ya usalama barabarani au kuwekwa mahabusu na kuandaliwa mashtaka na kupelekwa mahakamani au vyote kwa pamoja.

Aidha, amesema kuwa ni kosa kisheria kufunga taa zenye mwanga mkali zinazoongezwa kwenye magari au pikipiki yaani spot light na led bar wanafunga kama urembo kwenye magari na pikipiki na wanatakiwa wavitoe mara moja kwani wamefunga kwa kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani.

"Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani litafanya oparesheni kali kudhibiti ufungwaji wa taa zinazoongezwa kwenye magari na pikipiki, kuna watu wanaweka Taa za kuongezwa kwenye magari, nyuma ya magari makubwa hususani malori, wananchi wenye tabia hii waache mara moja kwani ni kinyume cha sheria"amesema Kamanda Ng'anzi.

Ameongeza pia ni kosa kisheria gari au pikipiki kubandikwa namba bandia zisizo na usajili, ambapo baadhi ya watu wamejenga utamaduni ambao wanajihalalishia kuwa ni sheria kuweka namba bandia kwenye magari, hivyo wanatakiwa watoe mara moja namba hizo kabla ya oparesheni kuanza.

Sambamba na hayo, amesema kunavmagari ambayo yamewekwa taa kutoka kiwandani hizo zinaruhusiwa kisheria mfano magari ya mgodini tu na kwenye mapori wakati wa uwindaji na sivyenginevyo, hivyo anapotoka maeneo hayo aweke kava za kuzuia mwanga mkali barabarani kwani mwanga huo unaweza kusababisha uoni hafifu.

Comments