Skip to main content

THE ROYAL TOUR IMELETA MAPINDUZI KATIKA UTALII-CC NGORONGORO

 

THE ROYAL TOUR IMELETA MAPINDUZI KATIKA UTALII-CC NGORONGORO


Na Mwandishi Wetu

Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Richard Kiiza amesema filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii ambapo mpaka kufikia nusu mwaka wa fedha wa 2023/2024 Mamlaka hiyo imeweza kutembelewa na watalii 534,065.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es salaam Kamishna Kiiza amesema matarajio ya mamlaka hiyo hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2023/2024 idadi ya wageni watakaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro watafikia milioni moja ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita ambapo wageni kwa mwaka nzima walikuwa 752,232.

Kamishna Kiiza amesema ongezeko hilo la wageni linakwenda sambamba na kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ambapo mpaka kufikia nusu ya mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi bilioni 123 tayari zimeshakusanywa.

Ameeleza kwamba kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuimarisha usimamizi wa Hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali ambayo itawawezesha watalii kutembelea maeneo ya utalii bila changamoto.

Kuhusu zoezi la kuhama kutoka ndani ya Hifadhi kwa hiyari kuelekea katika Kijiji cha Msomera na maeneo mengine Kamishna Kiiza amesema zoezi hilo linaendelea vizuri kutokana na wananchi wengi kuwa na hamasa ya kutaka kuhama hasa ikizingatiwa kuwa mamlaka imeendelea kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuboresha maisha yao nje ya Hifadhi.

Baadhi ya wahariri katika mkutano huo wameipongeza serikali ya awamu ya sita katika kusimamia zoezi hilo na kusema kwamba nguvu kubwa inahitajika kupambana na wale wote wanaotaka kudhoofisha juhudi hizo za serikali zenye lengo la kuimarisha maisha ya wananchi na kulinda Hifadhi.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Thobias Makoba ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kushirikiana kwa karibu na ofisi hiyo hivyo kurahisisha mchakato wa kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi.

Bw. Makoba amesema ofisi hiyo imejipanga vizuri katika kuhakikisha kila Mamlaka iliyo chini yake inafanya vikao vya mara kwa mara na waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Katika kikao hicho Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iliweza kutoa taarifa kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusiana na mafanikio ya serikali ya awamu ya sita yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani Machi, mwaka 2021.

Comments