ACT WAZALENDO YASHAURI TUME MPYA HURU YA UCHAGUZI KUANZA KAZI, YADAI KUWEPO KWA DOSARI KADHAA CHAGUZI ZA MARUDIO

 




NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM 


CHAMA Cha ACT Wazalendo kimeshauri kuanza kwa muundo na utaratibu mpya ya kuundwa kwa tume mpya ya Uchaguzi inayopatikana kwa utaratibu wa ushindani.


Hayo yamesemwa jijini Dar Es Salaam na Makamo mwenyekiti wa chama hicho bara,Isihaka Mchinjita alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali ikiwemo chaguzi ndogo za udiwani katika kata 23 zilizofanyika March 20 mwaka huu.


Mchinjita amesema chama hicho kimekuja na ushauri wa kuanza kwa tume hiyo huru ya Uchaguzi kutokana na kuonekana kwa dosari kadhaa katika uchaguzi huo ikiwemo wapiga kura kuwa wengi kuliko idadi ya walioandikishwa na baadhi ya wagombea wao kudaiwa kutekwa na kupigwa.


Amesema kupitia muswada wa Sheria ya tume ya  Uchaguzi ambao umepitishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inabidi tume ya Sasa ijiuzulu ili kupisha tume mpya huku akishauri tume hiyo mpya kuanza kuwa na watumishi wake kuanzia ngazi za juu mpaka ngazi za Halmashauri.


Aidha ameongeza kuwa serikali ya awamu ya SITA inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ijipambanue kwa vitendo kwenye kusimamia demokrasia  kupitia chaguzi hizi za marudio ili kupatikana kwa viongozi sahihi na waliochaguliwa na wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa vitongoji na vijiji Pamoja na ule Mkuu unaotarajia kufanyika mwaka 2025.


"Ndugu waandishi wa habari sisi ACT Wazalendo pia tunashauri utaratibu wa uzalishaji,uhifadhi na usambazaji wa karatasi za kupigia kura kuangaliwa upya Ikiwemo kushirikisha vyama vya siasa na wadau wengine kwenye kila hatua ili kuepusha sintofahamu, Hali inayopelekea wagombea wengine kulalamika kuibiwa kura"amesema Mchinjita.


Hata hivyo chama hicho pia kimeshauri mapendekezo yaliyoainishwa na Tume ya Haki jinai yafanyiwe Kazi ili kuvifanyia maboresho vyombo vya ulinzi na usalama hasa jeshi la polisi katika kusimamia haki za wananchi kwa weledi na usawa huku kikishauri pia uamuzi Uliopitishwa na Bunge February 2 mwaka huu kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na Tume huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI uheshimiwe.

Comments