Skip to main content

JESHI LA POLISI LAKAMATA WEZI SUGU WA PIKIPIKI DAR.

 

JESHI LA POLISI LAKAMATA WEZI SUGU WA PIKIPIKI DAR.



Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam

NA ABRAHAM NTAMBARA

JESHI la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam linaendelea na operesheni kali maalum  ya kuzuia vitendo vya kihalifu na  kukamata watuhumiwa mbalimbali wakiwemo wezi wa pikikipi na kukamata  pikipiki  zilizoibwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 5 jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amesema Operesheni hiyo ilianza tarehe 06 Februari 2024 na inaendelea mpaka sasa imemkamata Omari Mlopa (28) mkazi wa Mlandizi na wenzake wawili wakiwa na pikipiki 32 zilizoibwa  na baadae kuzifanya zao kwa kuzikodisha kwa mikataba kwa watu mbalimbali na kujipatia pesa kila siku.

“Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi Kanda maaluma ya Dar es Salaam umebaini kuwa watuhuhumiwa hao walibadilisha namba za usajili za pikipiki hizo na kuweka  namba bandia ili  zisitambulike. Pikipiki 13 tayari zimetambuliwa na wamiliki,” amesema SACP Muliro.

Wakati huo huo Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam  linaendelea operesheni maalum ya  ukamataji wa watu wanaokiuka sheria kwa kutenda  makosa ya usalama barabarani hasa  kwa waendesha pikipiki (Bodaboda) na Bajaji.

Kwamba katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2023 makosa ya pikipiki yaliyokamatwa ni 179,174, walioandikiwa faini za papo kwa hapo ni 178,937, waliofikishwa Mahakamani ni 237, waliohukumiwa adhabu ya kulipa faini 236, na mmoja alihukumiwa kifungo jela

Kwa kipindi cha Januari hadi Februari 2024 makosa ya pikipiki yaliyokamatwa  36,775, walioandikiwa faini za papo kwa hapo ni 36,754, waliofikishwa mahakamani ni 14, na mashauri 7 yapo kwenye ofisi ya Mashitaka ya Taifa.

Katika Operesheni hii baadhi ya makosa ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa  mara kwa waendesha pikipiki na bajaji ni kutovaa kofia ngumu, kupita taa nyekundu, ulevi, kuzidisha abiria, kupita barabara za mabasi yaendayo haraka pamoja na kupakia abiria kwenye taa za kuongozea magari.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam licha ya kuendelea kutoa elimu  juu ya  uzuiaji wa makosa, ukamataji umelenga pia watu ambao wamekuwa wakikaidi na kutotii sheria kwa kuendesha vyombo vya moto bila kujali na baadae kujikuta wakisababisha ajali. 

Comments