WATANZANIA KUANZA 'KUENJOY' SAFARI ZA TRENI YA SGR KUANZIA JULAI 2024.
WATANZANIA KUANZA 'KUENJOY' SAFARI ZA TRENI YA SGR KUANZIA JULAI 2024.
Na PrayGod THADEI,Dar Es Salaam/Morogoro
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la reli nchini TRC,Masanja Kadogosa amesema mpaka mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu,Usafiri wa treni ya kisasa ya umeme ya SGR kutoka Dar Es Salaam mpaka Dodoma utakuwa umekamilika na kuanza safari zake.
Kadogosa ameyasema hayo wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya bunge uwekezaji na mitaji ya umma,PIC ilipofanya ziara ya ukaguzi wa treni hiyo ya umeme kutoka jijini Dar Es Salaam mpaka Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi huyo amewahakikishia wananchi kuwa mradi huo umeunganishwa kupitia vyanzo mbalimbali vya umeme nchini,hivyo hitilafu yoyote ya umeme haiwezi kuwa kikwazo Cha kukwamisha mradi huo ikiwemo safari za treni hiyo ya kisasa.
Kuhusu suala za nauli za abiria watakaopanda treni hiyo,Kadogosa amesema tayari wao Kama shirika walishatoa mapendekezo yao kwa Mamlaka ya udhibiti wa Usafiri ardhini,Latra ambayo yalizingatia pia gharama za uendeshaji (running cost)wa treni hiyo ya kisasa,hivyo wakati wowote nauli za Usafiri huo zitatangazwa na Latra kwani mazungumzo yalihusisha wadau wote.
"Kama mnavyoona hapa leo kamati yetu ya bunge imesafiri katika safari ya Majaribio ya treni hii ya SGR,kutoka Dar mpaka hapa Morogoro ambapo kipande chake kimekamilika kwa asilimia kubwa,hivyo Kama Mheshimiwa RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan alivyotutaka kuanza kutoa huduma zetu mpaka kufikia mwezi Julai kipande Cha kutoka hapa mpaka Dodoma kitakuwa kimekamilika na tunategemea kunza safari kuanzia jijini Dar Es Salaam mpaka Dodoma" aliongeza Kadogosa.
Kwa upande wake Makamo Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge,uwekezaji na mitaji ya umma,PIC Mhe Augustine Vuma ameupongeza hatua za Shirika Hilo kwa uwekezaji uliofanyika kwani matunda ya fedha zilizowekezwa yataanza kuonekana Mara baada ya mradi huo kuanza Kazi rasmi.
Amesema serikali imefanya mradi mkubwa Sana na usimamizi wa mradi huo umekuja na matokeo chanya ambapo thamani ya fedha iliyowekezwa inaonekana.
"Jambo la kwanza Kama kamati tumeridhishwa pasipo na shaka kwamba huu mradi umetekelezwa katika viwango ambavyo vinastahili,na ni mradi unaovutia kwa watanzania na tumeelezwa kuwa miongoni mwa faida za huu mradi katika utekelezaji wake tu umeshatoa ajira za moja kwa moja elfu thelathini,na zisizo za moja kwa moja zaidi ya Laki moja na nusu ambazo zimewezesha kipato Cha zaidi ya bilioni 350"alisema Makamo Mwenyekiti huyo wa PIC.
Aidha ameongeza kuwa Usafiri huo wa treni ya kisasa ya umeme utakwenda kusaidia watanzania kwani utapunguza zaidi ya nusu ya masaa ambayo mabasi hutumia kusafirisha abiria hivyo watanzania wataitumia muda mfupi kusafiri na gharama za usafirishaji wa Mizigo zitapungua kwa asilimia zaidi ya 40 huku akitoa Rai kwa TRC kuendelea kutunza miundombinu hiyo ya reli ya kisasa na kuwasimamia wakandarasi kwa Kazi ambazo zimesalia katika vipande vya reli vilivyokamilika na wale ambao wanaendelea na ujenzi wa mradi huo kwa vipande vingine.
Comments