ELIMU YA FEDHA MBIONI KUINGIZWA KATIKA MFUMO RASMI WA ELIMU NCHINI, lengo kuwawezesha vijana kuwa na nidhamu ya kusimamia fedha
ELIMU YA FEDHA MBIONI KUINGIZWA KATIKA MFUMO RASMI WA ELIMU NCHINI, lengo kuwawezesha vijana kuwa na nidhamu ya kusimamia fedha
Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akifungua warsha warsha kuhusu uchopekaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu iliyowakutanisha viongozi mbalimbali na taasisi na elimu ya juu nchini.
Naibu Gavana Benki Kuu ya Tanzania Sauda Msemo akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu kwa viongozi wa vyuo mbalimbali nchini ili kujadili mitaala ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wa elimu ya juu Jijini Dar es Salaam.
Matukio mbalimbali katika picha katika ufunguzi wa warsha kuhusu uinngizaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu inayofanyika jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amesema Serikali itahakikisha elimu ya fedha inaingizwa kwenye mfumo rasmi wa elimu na kuanza kufundishwa nchini.
Kipanga amebainisha hayo leo Aprili 17, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya siku tatu kuhusu uinngizaji wa elimu ya fedha katika mitaala ya elimu ya juu iliyowakutanisha viongozi mbalimbali na taasisi za elimu ya juu nchini ambapo jambo hilo litatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Seyansi na Teknolojia na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Amebainisha kuwa elimu hiyo itatolewa katika vyuo vikuu lengo likiwa ni kuwawezesha vijana kuwa na uwezo wa kuwa na nidhamu ya kusimamia fedha, kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii.
“Wizara tutahakikisha elimu ya fedha inafundishwa katika mfumo wa elimu nchini hivyo twende kwa haraka kuhakikisha vijana ambao ni sehemu ya jamii nchini wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha hivyo natarajia wakuu wa vyuo mtabeba uelewa huo muhimu kwa vyuo vyetu nchini,” amesema Kipanga.
Naibu Waziri Kipanga amebainisha kuwa, BoT, itaendelea kusimama na vyuo na taasisi za elimu na Wizara ya Elimu katika kuhakikisha dhana ya elimu hiyo inakuwa endelevu na inafundishwa katika ngazi za jamii hata kwa wale walio nje ya mfumo rasmi wa elimu nchini.
Ametumia fursa hiyo kuviagiza Vyuo Vikuu nchini kushirikiana na BoT kufanya tathmini ya utekelezaji wa mpango huo ili kuboresha mbinu na nyenzo za kufikisha ujumbe huo kwa jamii.
Hivyo amesema baada ya tathmini hiyo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipatiwe taarifa ili isaidie katika kufanya maamuzi kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga uelewa wa masuala ya fedha kwa jamii.
Kwa upande wake Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo amesema elimu ya fedha inakuwa ni sehemu ya masomo, kwmaba somo hilo liingizwe kwenye mfumo ya elimu msingi hadi vyuo vikuu.
Kwamba April mwaka jana, BoT iliwashirikisha wakuu wa taasisi za Elimu ya Juu nchini, kwa uwakilishi wa wakuu wa vyuo vikuu pamoja na TCU na NACTIVET kwa lengo la kukubaliana juu ya azma ya kufundisha somo la elimu ya fedha ngazi ya elimu ya juu nchini.
“Hadi hivi sasa taasisi tatu za elimu ya juu zimechukua hatua za kuingiza somo la elimu ya fedha katika mitaala yao, hivyo warsha hii ni kuchochea uwepo wa elimu ya fedha kwa vyuo vingi nchini kuendana na mabadiliko ya mageuzi ya kiuchumi nchini,”amesema Msemo.
Msemo ameeleza kwamba, takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonesha takribani watu asilimia 34.5 ni vijana walio na umri kati ya miaka 15-35 hivyo ili kuleta tija na ufanisi katika masuala ya uchumi, ujuzi na uzoefu wa masuala ya fedha ni moja ya sifa muhimu kufikia azma hiyo.
Amesema elimu hiyo ya fedha kwa Watanzania itachochea maendeleo kwa kuongeza utumiaji rasmi wa huduma za fedha na kuwawezesha watu wengi kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi na kukuza uchumi kwa ujumla.
Sauda amesema elimu kwa vijana wa vyuo vikuu itawasaidia kuweka akiba, kupanga bajeti na kufanya uamuzi wa masuala ya fedha kwa kuzingatia viashiria hatarishi na kuelewa taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za fedha ili kufanya maamuzi sahihi ya fedha ili waitawale.
"Tunatarajia kujenga ‘displine’ ya fedha kupitia elimu ya fedha kwani watakuwa na uwezo wa kutawala fedha sio fedha kuwatawala vijana hao,” ameongeza Msemo.
Kadhalika amesema BoT kwa kushirikiana na wadau wengine wa Baraza la Huduma Jumuishi za Fedha, imetoa muongozo na mtaala wa elimu ya fedha kwa wakufunzi ambao utatumika na taasisi za elimu ya juu kwa kuwafundisha watoa huduma za elimu ya fedha kuwafikia wananchi wote walio nje mfumo wa elimu.
“Tayari tumeingia makubaliano na baadhi ya taasisi zaa elimu katika mtaala huo wa kufunzi wa fedha na tulioingia nao makubaliano ni Chuo Kikuu cha Iringa, Zanzibar, Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania ,” ameseama.
Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA), Felix Adam amesema warsha hiyo ni muhimu kwake kwa sababu hayo maeneo yanayojadiliwa yatawasaidia kuwapa elimu ya fedha wahitimu wao.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments