Skip to main content

JESHI LA POLISI LATOA UFAFANUZI KIFO CHA BABU G, WALIOTOA TAARIFA ZA UONGO KIKAANGONI

 

JESHI LA POLISI LATOA UFAFANUZI KIFO CHA BABU G, WALIOTOA TAARIFA ZA UONGO KIKAANGONI


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Gunda Asheri ambaye ni shemeji wa marehemu Robart Mushi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

NA MWANDISHI WETU 

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa ya uongo na uzushi inayosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na kifo cha Robart Mushi maarufu kama Babu G. ambaye picha yake imeambatanishwa kwenye taarifa hizo kuwa alipotea Aprili 11, 2024 na baadae kugundulika katika Chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Polisi Kilwa Road huku ikidaiwa Polisi kuhusika na kifo hicho kwa kumuua.

Aakizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23, 2024 jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amesema kuwa mtu huyo alifariki baada ya kugongwa na gari wakati akivuka barabara.

"Ukweli ni kwamba tarehe 11 Aprili, 2024 majira ya saa 10 Alfajiri Askari Polisi wa Usalama  barabarani alipewa taarifa na mwananchi kuwa eneo la Taa za kuongozea magari za Buguruni, Ilala  mtu mmoja mwanaume aliyekuwa akivuka  barabara eneo hilo la Kimboka kuelekea Chama aligongwa na gari ambalo halikusimama (hit and Run), " amesema SACP Muliro na kuongeza,

"Mtu huyo alipata majeraha makubwa kichwani, kifuani na eneo la chini la mgongo na kisigino cha mguu wa kulia. Eneo hilo lina watu wengi ambao wanakesha kwa biashara mbalimbali na walishuhudia tukio hilo,". 
 
Kwamba baada ya tukio hilo, mtu huyo alipelekwa haraka Hospitali ya Amana na Polisi,  lakini baada ya kumfikisha Madaktari walibaini kuwa mtu huyo alikuwa tayari amekwisha fariki, Kwa sababu chumba cha kuhifadhi maiti  cha hospitali ya Amana kilikuwa hakina nafasi ,ilishauriwa akahifadhiwe kwenye Hospitali ya Jeshi la Polisi iliyo barabara ya Kilwa Temeke ambayo inatoa huduma hata kwa raia kuhusiana na suala hilo.

Amebainisha kuwa Aprili 21, 2024  ndugu wa marehemu walipatikana na wakautambua mwili wa ndugu yao kwani hakuwa na kitambulisho wala simu, hivyo taratibu za mwisho za mazishi zinafanywa ili akazikwe. 
   
"Kutokana na taharuki iliyotengenezwa na kujengwa kwa makusudi na mtu anayejiita Malisa gj na Bonoface Jacob ambao kwenye “post” zao walionesha nia ya wazi ya kutengeneza chuki dhidi ya Polisi na Serikali kwa  wananchi kuwa mtu huyo aliyepata ajali alikuwa ameuawa na Polisi , Kitendo kilichofanywa na watu hao ni kosa kisheria na hakivumiliki na lazima Jeshi lichukue hatua za kisheria dhidi ya wahusika ikiwa ni pamoja na kuwakamata , kuwahoji  kwa kina na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo," ameeleza SACP Muliro.

SACP Muliro amesemaa Jeshi la Polisi halitavumilia watu ambao wanaibuka na taarifa za uongo na uzushi ambazo zinalenga kujenga chuki na taharuki kwa wananchi, kwamba Jeshi litaendelea kusimamia misingi ya kisheria na halitakuwa na huruma kwa mtuhumiwa yoyote wa kihalifu na litamshughulikia haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa sheria. 

Kwa upande wake Gunda Asheri ambaye ni Shemeji wa Marehemu amethibitisha kupatikana kwa mwili wa ndugu yao huyo na kuthibitisha kuwa alifariki baada ya kugongwa na gari na sio kama inavyoelezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa aliuawa na Jeshi la Polisi.

Amesema kuwa hawahusiki na taarifa hizo zinazolenga kuwachonganisha wao kama familia na Jeshi la polisi na kueleza kuwa kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuuchukua mwili huo kwa ajili ya kuendelea na mazishi.

Comments