KAMISHNA WA ARDHI DAR,PWANI AWATAKA WANAODAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI KULIPA MARA MOJA,ATOA MAAGIZO KWA HALMASHAURI

 KAMISHNA WA ARDHI DAR,PWANI AWATAKA WANAODAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI KULIPA MARA MOJA,ATOA MAAGIZO KWA HALMASHAURI 

Kamishna wa ardhi msaidizi,Dar Es Salaam na Pwani Shukra Kyando akizungumza na waandishi wa habari Leo May 11,2024 Jijini Dar Es Salaam 



Na PrayGod THADEI,Dar Es Salaam 

Siku moja Mara baada ya Wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutoa siku 30 kwa wadaiwa wote wa Kodi ya pango la Ardhi kulipa Kodi hiyo,hii Leo  kamishna wa ardhi msaidizi Mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani Shukra Kyando amezitaka Halmashauri zote za Wilaya za Dar Es Salaam na Pwani kutoa huduma kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 2 usiku kama Wizara ilivyotoa agizo ili wananchi wengi wapate muda wa kulipa Kodi ya ardhi.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo jijini Dar Es Salaam Kamishna msaidizi,Kyando amesema Mara baada ya agizo la Waziri wa ardhi hapo jana ni vyema Sasa Ofisi za ardhi za halmashauri  zote wakatoa huduma hadi saa mbili za usiku siku zote za kazi kuanzia tarehe ya Tangazo ili kuwahudumia wananchi kwa urahisi kabla ya tamati ya zoezi hilo.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya ardhi kila mmiliki wa ardhi anapaswa kulipa Kodi ya pango la ardhi kwa mkupuo au kwa awamu kila mwaka hivyo ni muda muafaka kwa wanaomiliki ardhi Mikoa ya Dar Es Salaam na Pwani kulipa Kodi zao kabla ya tarehe ya mwisho ya kulipa Kodi hiyo ili kuepuka hatua ambazo wanaweza kuchukuliwa ikiwemo kufikishwa mahakamani na ardhi zao kumilikishwa watu wengine au kuuzwa kwa nyumba zao ili serikali ipate hela ya kufidia gharama ambazo mmiliki hakulipa kama Kodi ya Pango la ardhi kwa kipindi chote anachodaiwa.

"Kwa mujibu wa fungi la 50 la Sheria ya Ardhi (sura ya 113)wamiliki watakaokaidi kulipa pango la Ardhi watafikishwa mbele ya mahakama na kwa mujibu wa fungu la 45 la Sheria ya Ardhi,taratibu za kisheria za ubatilisho wa Miliki zao zitaendelea" amesema Kyando.

Aidha amewataka wananchi wanaodaiwa Kodi ya pango la Ardhi kulipa Kodi hizo kwa urahisi kwani wanaweza kulipa hata wakiwa nyumbani kwa Kupiga *152*00# ambapo watapata maelekezo yote ya jinsi ya kulipa Kodi hizo ikiwemo kupewa 'control number' ambazo watalipa kwa njia ya simu au kwa njia ya Benki.

Hata hivyo Kyando ametoa Rai kwa wananchi watumie njia walizoelekezwa na Wizara ikiwemo kujikadiria wao kiwango Cha Kodi wanayotakiwa kulipa na kuzilipa Kabla ya tarehe husika ya mwisho ya kulipa Kodi hiyo ambapo Jana May 10,Wizara ilitoa siku 30 pekee.

Kwa upande wake Afisa Ardhi mwandamizi kitengo Cha Kodi Dar Es Salaam na Pwani,Seif Mahiza amesema wadaiwa wa Kodi ya Pango la Ardhi pia wanaweza kulipa Kodi zao kwa kutembelea tovuti (website) ya Wizara ya Ardhi,Nyumba na maendeleo ya Makazi ambapo watapata taratibu zote za jinsi ya kulipa Kodi zao.

Aidha amesema pia kama wadaiwa wa Kodi ya Pango la Ardhi watashindwa kutumia simu zao au kutembeleana tovuti ya Wizara pia wanaweza Kufika katika Ofisi za Wizara ya Ardhi zilizopo mtaa wa Magogoni Jijini Dar Es Salaam au Kufika Katika Ofisi za Ardhi Katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani.
Afisa Ardhi mwandamizi kitengo Cha Kodi Dar Es Salaam na Pwani, Seif Mahiza akizungumza katika mkutano huo wa waandishi wa Habari


Comments