TMA YATOA MWELEKEO WA HALI YA HEWA MSIMU WA KIPUPWE, baridi na joto la wastani vyatajwa.
TMA YATOA MWELEKEO WA HALI YA HEWA MSIMU WA KIPUPWE,
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Ladislaus Chang’a (picha na maktaba).
NA MWANDISHI WETU
MAMLAMA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa Hali ya Hewa kwa Mwezi Juni hadi Agosti 2024 ambapo katika kipindi cha msimu wa Kipupwe inatarajiwa hali ya baridi ya wastani na joto kiasi katika maeneo mengi ya nchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 27, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa TMA Dkt. Ladislaus Chang’a imeeleza kuwa, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi, kusini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na kanda ya kusini ambapo vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai.
Aidha Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 20 oC.
Kwa upande wa Ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 23oC na 26oC kwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani, na kati ya nyuzi joto 17oC na 23oC katika maeneo ya nchi kavu huku maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 17oC
Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 20 oC huku, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 15 oC.
Kanda ya magharibi (Mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma) hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 15 oC na 20 oC na, maeneno ya kusini mwa mkoa wa Katavi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali chini ya nyuzi joto 15oC.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma)Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 11oC na 17oC.
Ukanda wa pwani ya kusini (Mikoa ya Mtwara na Lindi) Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 17 oC na 22 oC.
Kanda ya kusini (Mkoa wa Ruvuma) Hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10oC na 18 oC.
Nyanda za juu kusini-magharibi (Mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro) Hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 7 oC na 15 oC. Hata hivyo, katika maeneo yenye miinuko, kiwango hicho kinatarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 7 oC.
Kwa kawaida msimu wa Kipupwe hutawaliwa na upepo wa kusi. Hata hivyo, msimu wa Juni hadi Agosti, 2024 unatarajiwa kuwa na upepo wa wastani hadi upepo mkali utakaovuma kutoka kusinimashariki na vipindi vichache vya upepo wa kusi katika ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu. Kwa ujumla, upepo wa wastani unatarajiwa kushamiri katika maeneo mengine ya nchi.
Kwa msimu wa Kipupwe Juni hadi Agosti kinatawaliwa na hali ya ukavu katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo, vipindi vichache vya mvua vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita, Simiyu na Mara), kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, nyanda za juu kaskazini-mashariki (mikoa ya Arusha na Kilimanjaro) pamoja na ukanda wa pwani (mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).
Katika kipindi cha msimu wa Kipupwe, 2024, hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya kati ya bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuwa ya wastani hadi chini ya wastani, ikiashiria kuelekea hali ya La NiƱa hasa mwisho wa msimu. Hali hii inatarajiwa kuwa na mchango hafifu katika mifumo ya mvua hapa nchini.
Kwa upande wa Bahari ya Hindi, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa kuendelea kuwepo katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika Mashariki) ikilinganishwa na joto la Bahari upande wa mashariki mwa Bahari ya Hindi (Pwani ya Indonesia). Hali hii inatarajiwa kuimarisha mifumo inayosababisha mvua katika maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi na maeneo jirani.
Hata hivyo Tahadhari za kiafya zinapaswa kuchukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi. Kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi katika kipindi hicho, maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa.
Aidha, wakulima wanashauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiki cha msimu wa Kipupwe. Hata hivyo, sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinaweza kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho hivyo Watumiaji wa taarifa za utabiri wanashauriwa pia kufuatilia na kuzingatia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa kama zinavyotolewa na TMA.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments