Bodi Ya Mikopo Elimu Ya Juu Yaja Na #Fichua Kuwasaka Wadaiwa Sugu

 Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu Yaja Na #Fichua Kuwasaka Wadaiwa Sugu




Dar Es Salaam 

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Ijumaa, Juni 28, 2024) imezindua Kampeni Maalumu inayolenga kuwashirikisha wananchi kwa kutumia simu na mitandao ya kijamii, kuwafichua wadaiwa sugu wa mikopo ya elimu ya juu.

Kampeni hiyo, inayofahamika kama #Fichua imezinduliwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dkt. Bill Kiwia ambaye amesema kampeni hiyo itaendeshwa kwa miezi miwli kuanzia leo, Juni 28.

Dkt Kiwia amesema Kampeni hii inalenga kuwashirikisha wananchi kutimiza jukumu la kizalendo la kuwafichua wadaiwa wa HESLB wenye kipato lakini hawajitokezi na kuanza kurejesha mikopo yao.

“Tumeipa jina la #Fichua – KUWA HERO WA MADOGO ili kuhamasisha wananchi kushiriki katika urejeshaji wa mikopo iliyoiva ili iwanufaishe wengine – hatua ambayo bila shaka itawawezesha vijana wengi zaidi kupata elimu ya juu na wewe mwananchi kuwa SHUJAA wao,” ameongeza Dkt. Kiwia.

Amesema Ili kutoa taarifa za wadaiwa, mwananachi anapaswa kutuma majina ya mnufaika, chuo alichosoma, eneo analofanya kazi, jina la kampuni anayofanyia kazi au anayomiliki na eneo ilipo kampuni hiyo.

Ameongeza kuwa mwananchi anashauriwa kutuma taarifa hizo kwa barua pepe (fichua@heslb.go.tz); kutuma ujumbe wa WhatsApp (0739 66 55 33); kupiga simu kwenda 0736 66 55 33 kati ya saa 2:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

Njia nyingine ni pamoja na kutembelea tovuti www.heslb.go.tz na kuwasilisha taarifa kupitia kiunganishi cha ‘e-Mrejesho’. Pamoja na njia hizi, wananchi pia wanaweza kutuma ujumbe (DM – Direct Messages) kwenda Instagram, X (zamani Twitter) au Facebook kwa jina la ‘HESLB Tanzania’ LILILOTHIBITISHWA na lenye ‘blue tick’.

                                        Maoni ya wadau-wanafunzi

Akizungumzia kampeni hiyo, Japhet Makyao, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya Udaktari na Upasuaji katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala – Tanzania (KIUT) ameipongeza HESLB kwa ubunifu huo na kuwataka wadaiwa sugu wenye vipato kurejesha.

“Ukweli ni kuwa, mimi hadi sasa hivi mwaka wa tatu, bila Bodi ya Mikopo, nisingeweza kufika hapa … ningependa kuona waliowezeshwa kusoma na wana kipato, wajitokeze ili vijana wengine kama mimi wanufaike,” amesema Japhet mara baada ya uzinduzi huo.

Kwa upande wake, Khadija Sultan, mwanafunzi wa mwaka pili, Shahada ya Usimamizi wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Tumaini – Dar es salaam (DarTU) ameishukuru Serikali kwa kumuwezesha kusoma na kuwaomba wadaiwa kumaliza kurejesha mikopo yao.

“Mimi ni yatima, nimepoteza wazazi wangu wote wawili nikiwa bado mdogo sana, bila Serikali nisingeweza kusoma kabisa … hivyo ninawaomba wale ambao hawajaanza kurejesha, au wanaorejesha kwa wasiwasi kuanza kurejesha,” amesema Khadija.


Story na HELSB

 

Comments